Watu kadhaa wameuawa katika msururu wa ghasia kati ya jamii katika eneo linalozozaniwa nchini Sudan Kusini, shirika la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na dharura OCHA na afisa wa eneo hilo walisema Jumatano.
OCHA imesema mapigano katika eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Abyei kwenye mpaka na Sudan yamesababisha vifo vya watu 36 kufikia Machi 6, huku idadi isiyojulikana wakijeruhiwa na wengine 50,000 wakiripotiwa kuhama makazi yao.
“Mivutano baina ya jamii iliongezeka katika wiki za hivi karibuni katika Eneo la Utawala la Abyei (AAA), linalodaiwa kuchochewa na mizozo ya muda mrefu ya eneo, mivutano baina ya makabila na kutaka kulipiza kisasi,” shirika hilo lilisema katika taarifa.
Imesema mapigano hayo yamekuwa yakiendelea tangu Februari 10 lakini yalizidi mapema mwezi Machi, na kuongeza kuwa operesheni za kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa zilisitishwa na wafanyakazi wa kutoa misaada kuhamishiwa mahali salama.
Abyei imekuwa ikigombaniwa tangu Sudan Kusini ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka wa 2011, ingawa kumekuwa na mvutano kwa muda mrefu kati ya jamii ya Ngok Dinka na wafugaji wa Misseriya wanaovuka eneo hilo kutafuta malisho.
Msemaji wa eneo la utawala la Abyei Ajak Deng alisema mashambulizi mawili mabaya mwishoni mwa juma yalitekelezwa na wafugaji wa Misseriya na wanajeshi wa Sudan waliokuwa na silaha kali.
Alisema watu sita waliuawa Jumamosi na wengine 27 Jumapili, na kuongeza kuwa hali bado ni ya wasiwasi na watu bado wanaishi kwa hofu.
Balozi za Amerika mjini Juba na Khartoum zilitoa taarifa ya pamoja zikielezea “wasiwasi wao mkubwa” kutokana na kuongezeka kwa ghasia katika eneo hilo.
“Tunatoa wito kwa pande zote kukoma kulipiza kisasi na kurejea kwenye mazungumzo,” walisema.
Abyei imekuwa chini ya ulinzi wa Umoja wa Mataifa tangu uhuru wa Sudan Kusini, na Kikosi cha Usalama cha Muda cha Umoja wa Mataifa kwa Abyei (UNISFA) kilichotumwa huko pia kilielezea wasiwasi wake juu ya umwagaji damu.
“Hii imesababisha watu kupoteza maisha na kusababisha mateso mengi ya kibinadamu kwa watu pamoja na kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika kufikia kuishi pamoja kwa amani huko Abyei,” UNISFA ilisema katika taarifa yake Jumanne.