Serikali ya kijeshi ya Mali siku ya Jumatatu iliitaka Denmark kuondoa “mara moja” takriban wanajeshi 100 waliowasili hivi karibuni wa vikosi maalum vilivyotumwa nchini humo.
Serikali ya jeshi ambayo iliingia madarakani kwa mapinduzi mnamo Agosti 2020, ilisema katika taarifa kwenye Televisheni ya serikali na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba “wanajeshi hao walitumwa nchini humo bila idhini.”
Kikosi cha wanajeshi wapatao 90 wa Denmark kiliwasili Mali kujiunga na vikosi maalum vya Ulaya vinavyosaidia operesheni za kupambana na jihadi nchini humo, jeshi la Denmark lilisema wakati huo.
Wizara ya mambo ya nje ya Denmark ilisema katika taarifa yake Jumatatu kwamba “wanafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha utulivu ”na “wanawasiliana na serikali ya mpito ya Mali.”
“Kwa sasa kuna sintofahamu kubwa kuhusu tangazo la serikali ya mpito. Mchango wa Denmark ni sehemu ya operesheni inayoongozwa na Ufaransa nchini Mali, na kwa hivyo tunaratibu kwa karibu na kwa msingi unaoendelea na washirika wetu, ikiwa ni Ufaransa,” ilisema taarifa hiyo.
Kikosi hicho, ambacho kilitangazwa kutumwa kwake Aprili 2021, kiko Menaka mashariki mwa Mali
Mamlaka yake yalipaswa kuendelea hadi mwanzoni mwa 2023. Denmark hapo awali ilituma wanajeshi kushiriki katika kuweka amani nchini Mali, baadhi ya wanajeshi wake wakiwa na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MINUSMA na wengine na Operesheni ya Barkhane inayoongozwa na Ufaransa.
Kikosi kipya kinajiunga na Task Force Takuba — kikosi cha wanajeshi 900 kinachoongozwa na Ufaransa kilichozinduliwa Machi 2020.
Mataifa mengine ambayo yamechangia kwa kupeleka wanajeshi wake ni Uholanzi, Estonia, Sweden, Norway, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech, Ureno, Italia na Hungary.
Nchi za Ulaya zimeibua wasiwasi kuhusu kutumwa kwa mamluki kutoka kundi la Wagner la Urusi katika ardhi ya Mali na kuchelewa kwa Mali kurejea katika utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti 2020.