Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Malta imekuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuhalalisha matumizi ya bangi - Mwanzo TV

Malta imekuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuhalalisha matumizi ya bangi

Nchi ndogo ya Malta Jumanne imekuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuhalalisha matumizi ya bangi kwa mtu binafsi huku Ujerumani na Luxembourg zikitarajiwa kuchukua mkondo huo huo.

Ingawa nchi nyingi zimeharamisha utumiaji na umiliki wa bangi, na kuondoa vifungo vya jela kwa watumiaji, Canada, Uruguay na baadhi ya majimbo ya Amerika yamehalalisha utumizi wa bangi ikiwa ni pamoja kwa madhumuni ya matibabu.

Matumizi ya bangi katika maeneo mengine

Amerika ya Kusini

Uruguay ilikuwa nchi ya kwanza duniani kuhalalisha uzalishaji, usambazaji na utumizi wa bangi mwaka wa 2013.

Raia na wakazi wa Uruguay wanaweza kununua hadi gramu 40 za bangi kwa mwezi kutoka kwa maduka ya dawa, au kukuza mmea huo wenyewe nyumbani au hata kujiunga na vilabu vya bangi ambapo wanachama hukuza mimea hiyo kwa pamoja.

Serikali ya Uruguay imetoa leseni kwa kampuni mbili za kibinafsi kuzalisha na kusambaza bangi.

Nchi nyingine kadhaa za Amerika ya Kusini zimehalalisha matumizi ya bangi kwa matibabu: Chile ilihalalisha mwaka wa 2015, Colombia mwaka wa 2016 na Argentina, Mexico na Peru mwaka wa 2017.

Colombia iliidhinisha matumizi yake na kuuza kwa mataifa ya nje kwa madhumuni ya matibabu mnamo Julai huku mahakama za Mexico zikihalalisha matumizi ya kibinafsi.

Amerika ya Kaskazini

Mnamo 2018, Canada ikawa nchi ya pili duniani – na ya kwanza ya uchumi mkubwa wa G7 – kuruhusu matumizi ya burudani ya bangi.

Sheria iliyowekwa inaruhusu umiliki wa gramu 30 wa bangi na kukuza mimea minne kwa kila kaya.

Nchini Amerika, sheria ya shirikisho inakataza kukuza, kuuza na kutumia bangi.

Hata hivyo, majimbo 18 na mji wa Washington DC yamehalalisha bangi kwa matumizi ya burudani. California ndio soko kubwa zaidi duniani lililohalalisha uuzaji na utumizi wa bangi

Majimbo 36 na mji mkuu, Guam, Puerto Rico na Visiwa vya Virgin vya Amerika vimehalalisha bangi kwa madhumuni ya matibabu.

Ulaya

Chini ya sheria mpya ya Malta, watu wazima wataruhusiwa kuwa na hadi gramu saba za bangi na kukuza hadi mimea minne nyumbani.

Sheria hiyo pia inaruhusu vikundi vyenye wanachama 500 kuikuza kwa wanachama wao bila faida.

Serikali mpya ya Ujerumani pia imeapa kuhalalisha bangi kwa matumizi ya kibinafsi na Luxembourg inatarajiwa pia kuhalalisha ukuzaji wa mmea huo nyumbani ifikiapo mwaka ujao.

Uholanzi kwa ujumla, na Amsterdam haswa, yameruhusu uuzaji na utumiaji wa bangi katika maduka ya kahawa tangu 1976.

Nchi nyingine kadhaa za Ulaya zimehalalisha bangi kwa madhumuni fulani ya matibabu, ikiwa ni pamoja na Austria, Uingereza, Croatia, Ufini, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki, Italia, Macedonia Kaskazini, Poland, Romania na Slovenia.

Kwingineko

Mnamo 2018, mahakama kuu ya Afrika Kusini iliamua kwamba matumizi ya bangi ya kibinafsi kwa watu wazima ni halali. Thailand pia inapanga kuhalalisha kilimo cha bangi kwa madhumuni ya matibabu, ambayo itaifanya kuwa nchi ya kwanza Kusini-mashariki mwa Asia kuingia katika soko la uuzaji wa bangi  linalotawaliwa na Canada, Australia na Israeli.

Nchini Lebanon, ambako mashamba haramu ya bangi yameenea, bunge mwaka jana lilihalalisha kilimo cha bangi kwa matumizi ya kimatibabu.

Morocco, mzalishaji nambari moja duniani wa bangi ilipitisha sheria mwezi Machi iliyoidhinisha matumizi ya bangi kwa “matibabu, urembo na viwanda,” huku ikiweka marufuku hiyo.