Mamlaka Tanzania yaifungia Mwananchi kuchapisha habari mtandaoni kwa ‘ukiukaji wa kanuni’

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania (TCRA) imesitisha kwa muda huduma za mtandao za shirika la habari Mwananchi kwa madai ya  ‘ukiukaji wa kanuni’

Katika taarifa kwa  kwa umma TCRA imesema imesitisha leseni ya huduma za maudhui ya mtandaoni dhidi ya kampuni hiyo nchini Tanzania, kwa ukiukaji wa kanuni ya mwaka 2020 inayosimamia uchapishaji wa taarifa kwa mitadao za kijamii

TCRA imesema tarehe 01 Oktoba 2024, MCL ilichapisha maudhui mjongeo na sauti (audio-visual kwenye mitandao yake ya kijami, maudhui yaliyozuiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 16 ya Kanuni za Maudhui Mtandaoni za mwaka 2020.

”Maudhui hayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa taifa. Umma unaarifiwa kuwa, kufuatia kuchapishwa kwa maudhui yaliyokatazwa na yanayopingana na sheria, TCRA imesitisha kwa muda leseni za huduma za maudhui mtandano za Mwananchi Communication Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na Mwanaspoti) tangu tarehe ya kutolewa taarifa hii, wakati masuala mengine ya kiusimamizi yanafanyiwa kazi,’’ imeeleza taarifa ya TCRA , iliyotumwa kwenye mitandao yake ya kijamii

Kufuatia kuondolewa kwa leseni hiyo, MCL imetangaza kuondoa maudhui yake ya vibonzo kwenye mitandao yake ya kijami.

‘Uamuzi wetu wa kuondoa katuni unatokana na kusababisha tafsiri mbaya ambayo ni kinyume na nia yetu’’, taarifa hiyo iliongeza.

Kibonzo hicho yaliyoundwa na shirika la Mwananchi ni aina ya katuni ambayo ilikuwa ikionesha raia wa Tanzania wakilalama kwenye runinga juu ya matukio ya watu kutekwa na kuuawa . Katuni hiyo ilikuwa ikimuonesha mtu ambaye alikuwa akitizama runinga ambaye wengi wametafsiri kuwa ni Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan.

kwa siku za hivi majuzi Matukio ya watu kutekwa, kupotezwa na kuuawa katika mazingira ya kutatanisha yamezua wasiwasi nchini  Tanzania.