Mapigano yalizuka karibu na mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumanne, wakaazi na maafisa wa eneo hilo walisema, siku moja baada ya nchi jirani ya Rwanda kulishutumu jeshi la Congo kwa kulishambulia eneo lake kwa makombora.
Taarifa za machafuko hayo bado hazijafahamika, lakini wakazi kadhaa wa eneo karibu na mlima wa Mikeno, karibu kilomita 20 kaskazini mwa Goma, walisema walisikia milio ya risasi nzito asubuhi ya Jumanne.
“Baadhi ya wanajeshi wa Congo walishambuliwa,” alisema kiongozi wa mashirika ya kiraia ya eneo hilo Olivier Nzabonimpa, akiongeza kuwa shambulio hilo limewafanya wanakijiji kukimbilia Goma au kuvuka mpaka hadi Rwanda.
Boniface Kagumyo, meya wa wilaya iliyo karibu, alilaumu shambulio hilo kwa kundi la waasi la M23.
Wanamgambo wa M23 waliibuka kutoka kwa uasi wa Watutsi wa Congo mwaka wa 2013 ambao uliungwa mkono na nchi jirani za Rwanda na Uganda wakati huo.
M23 walianza tena mapigano mapema mwaka huu, wakiishutumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya mwaka 2009 ambapo wapiganaji wake walipaswa kujumuishwa katika jeshi.
Wengi nchini DR Congo wanashuku kuwa Rwanda inaendelea kuunga mkono kundi hilo.
Afisa mkuu wa jeshi la Congo katika eneo hilo, ambaye alikataa kutajwa jina, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mapigano hayo ya Jumanne yamegharimu maisha ya wanajeshi tisa wa Congo pamoja na 22 wa upande wa waasi.
“Tulikabiliana na waasi vikali, walikimbia kuelekea mpakani hadi kwenye makazi yao,” afisa huyo alisema na kuongeza kuwa vikosi vyake vilikamata sare na silaha za jeshi la Rwanda.
Mapigano hayo kaskazini mwa Goma yanakuja siku moja baada ya jeshi la Rwanda kusema kwamba makombora ya roketi kutoka kwa wanajeshi wa Congo yalishambulia maeneo ya ndani ya ardhi ya Rwanda na kuwajeruhi raia na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi yenye watu milioni 90, bado haijajibu madai hayo.