Sudan imejipata katika mgogoro baada ya jeshi kuchukua uongozi wa nchi na kutangaza hali ya hatari.
Sudan ni taifa lililoko kaskazini mashariki mwa Afrika likiwa limepakana na mataifa ya Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini. Lilitawaliwa na mkoloni Uingereza hadi mwaka 1956 lililpopata uhuru wake.
Sudan chini ya uongozi wa rais wa kwanza
Tangu uhuru, Sudan imekuwa ikitawaliwa na msururu wa serikali za mabunge zisizo imara na tawala za kijeshi. Mnamo Januari 1 1956, uchaguzi ulifanywa na Ismail al Azhari akachaguliwa kuwa Waziri mkuu wa kwanza wa Sudan.Kutoridhika na jinsi serikali ilivyokuwa ikiendesha shughuli zake , mapinduzi ya pili yalifanyika Mei 25 1969 na kiongozi wa mapinduzi Kanali Gafaar Nimeiry akawa Waziri mkuu, utawala wake mpya ulivunja bunge na kuharamisha vyama vyote vya siasa.
Tofauti zilizuka tena kati ya mirengo miwili tofauti ya uongozi na mapinduzi mengine yakafanyika mwaka wa 1971 yakiongozwa na chama cha Sudanese Communist Party. Siku kadhaa baadae, vikosi vya kijeshi vya kupinga ukomunisti vilimrejesha Nimeiry mamlakani.
Makubaliano ya Addis Ababa ya 1972 yalisababisha kusitishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kaskazini-kusini. Ila baadae mwaka wa 1976 kundi la kidini la kiisalmu la Ansar lilifanya jaribio la mapinduzi, kufikia 1979 aliyekuwa rais wakati huo Nimeiry alikutana na kiongozi wa Ansar Sadiq al- Mahdi ili kusitisha mapigano na kupata suluhu ya tofauti zao.
Mazungumzo ya viongozi hao ,yalisababisha kuachiwa kwa mamia ya wafungwa wa kisiasa na msamaha wa jumla ulitangazwa kwa wapinzani wote.
Sudan chini ya uongozi wa rais wa pili
Mnamo Juni 30 1989 kanali Omar al- Bashir aliongoza mapinduzi ya kijeshi. Serikali mpya ya kijeshi ilipiga marufuku vyama vya kisiasa na kuanzisha kanuni za kisheria za Kiislamu katika ngazi ya kitaifa.
Omar al- Bashir alitekeleza mauaji katika safu za juu za jeshi, akapiga marufuku vyama vya siasa na magazeti huru, na kuwafunga viongozi wakuu wa kisiasa na waandishi wa habari. Mnamo Oktoba 16 1993 alijiteua kuwa rais wa Sudan.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka wa 1969 Bashir alikuwa mgombea pekee kwa mujibu wa sheria za nchi aliyeruhusiwa kuwania kiti cha urais. Sudan ikawa nchi ya chama kimoja cha kisiasa cha National Congress Party (NCP).
Ili kupata suluhu ya matatizo ya kisiasa yaliyoikumba Sudan, spika wa bunge Hassan al- Turabi alimkaribisha Osama Bin Laden nchini Sudan.Amerika baadae ikaorodhesha Sudan kama nchi inayofadhili ugaidi. Sudan ilifanya bidii kuwaridhisha wakosoaji wake kwa kuwafukuza wanachama wa Jihad na kumhimiza Osama bin Laden kuondoka.
Kabla uchaguzi mkuu wa 2000 Hassan al -Turabi aliwasilisha muswada bungeni wa kupunguza nguvu za rais, Omar al – Bashir kwa upande wake akatangaza hali ya hatari akimshuku al -Turabi kwa kupanga mapinduzi dhidi yake, al –Turabi akafungwa jela.
Mnamo Februari 2003 chama cha Sudan Liberation Movement/Army (SPLM/A) na Justice and Equality Movement (JEM) kutoka Darfur walianza vita wakiishtumu serikali ya Sudan kwa kuwapendelea waSudan wenye asili ya kiarabu na kuwakandamiza waSudan weusi. Hali hiyo ilichangia kuzuka kwa vita vya Darfur ambapo takriban watu 300,000 waliuawa kati ya 2003 hadi 2008. Mahakama ya Kimatiafa ya Jinai ICC ikatoa agizo la kukamatwa kwa al- Bashir.
Mnamo Januari 9 2005, makubaliano ya Nairobi Comprehensive Peace Agreement yalitiwa saini kati ya serikali na chama cha SPLM/A, makubaliano hayo yalipelekea kufanyika kwa kura ya maoni ambapo kwa kauli moja wasudan wa kusini waliunga mkono kujitenga. Sudan Kusini ikajitenga rasmi na kuwa taifa huru Julai 9 2011.
Kufikia 19 Desemba 2018 maandamano makali yalianza Sudan kupinga ongezeko la bei za bidhaa na uongozi wa Omar al-Bashir ambaye alikuwa amekaa uongozini kwa miongo mitatu.
Serikali ililipiza kisasi na kuwakamata zaidi ya wapinzani na waandamanaji 800, wengine takriban 40 walifariki katika makabiliano na serikali. Serikali ya Omar al- Bashir ilipinduliwa mnamo Aprili 2019 na hali ya hatari ya miezi mitatu ikatangazwa.
Maandamano yalisitishwa baada ya muungano wa Forces for Freedom and Change (muungano wa makundi tofauti yaliyoongoza maandamano) na Transitional Military Council (serikali ya kijeshi) kutia saini makubaliano ya kuwepo kwa serikali ya mpito.
Sudan chini ya serikali ya mpito.
Baada ya makubaliano ya kisiasa kutiwa saini na Rasimu ya Tamko la Katiba la 2019, nyadhfa tofauti mpya zilizinduliwa ikiwemo kuundwa kwa taasisi na taratibu za mpito zilizojumuisha kuundwa kwa Baraza la pamoja la kijeshi na kiraia la Sudan. Kuwepo kwa Jaji Mkuu mpya wa Sudan kama mkuu wa tawi la mamlaka ya mahakama na kuwepo kwa Waziri mkuu mpya, nafasi hiyo ikamwendea Abdalla Hamdok.
Awali Abdalla Hamdok alifanya kazi katika Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika, aliapishwa Agosti 21. Septemba 3, Hamdok aliwateua mawaziri 14, ikiwemo Waziri wa kwanza mwanamke katika wadhfa wa Waziri wa masuala ya nje. Kufikia Agosti 2021, Sudan ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mpito Abdel Fattah al -Burhan na Waziri Mkuu Abdalla Hamdok.
Tarehe 21 Septemba 2021 Serikali ya Sudan ilitangaza majaribio ya mapinduzi yaliyoongozwa na jeshi, maafisa wa jeshi 40 walikamatwa.
Mapinduzi mengine yaliyoongozwa na afisa mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al – Burhan yalifanyika Jumatatu 25 Oktoba 2021.Waziri mkuu Abdallah Hamdok na mkewe walizuia nyumbani kwake Jenerali Al- Burhan na kuachiwa Jumanne jioni.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika na Ushirika wa Mataifa ya Kiarabu walilaani mapinduzi hayo.
Mapinduzi ya Jumatatu yamesababisha vifo vya takriban watu 8. Jenerali al- Burhan anasema mapinduzi hayo yalibidi kufanyika ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, akisisitiza kuwa uchaguzi wa kurejesha uongozi wa kiaria utafanyika Julai 2023.
Mapinduzi ya Jumatatu 25 Oktoba ni ya tano nchini humo.