Mashirika Ya Open Society Yalaani kufurushwa kwa Brian Kagoro kutoka Kenya

Mashirika ya Open Society yameilaani vikali serikali ya Kenya kwa kumzuia na kumkataza kuingia katika taifa hilo Mkurugenzi wake wa mipango Brian Kagoro, huku ikidai kwamba hakukuwa na kesi yoyote yaliyowasilishwa wala maelezo ya kimaandishi yaliyotolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Open Society, Brian Kagoro

Kagoro, wakili wa kikatiba wa Zimbabwe na mwanaharakati wa muda mrefu wa pan-African, alishikiliwa kwa zaidi ya saa 10 alipowasili uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kabla ya kuhojiwa na maafisa wa upelelezi na na kisha kuwekwa kwenye ndege kurudishwa Johannesburg, Afrika Kusini

Katika taarifa yake, Open Society ilisema Amri ya kumrudisha Nchini iliyoidhinisha shirika la ndege kumrudisha Afrika Kusini inamtaja kifungu cha 54 cha sheria ya uraia na uhamiaji ya Kenya ya 2011, kinachohusiana na makosa ya maswala ya stakabadhi. Shirika hilo lisisitiza kwamba Kagoro hana kosa lolote la ukiukaji sheria.

Pia shirika hilo limepinga  taarifa zilizomhusisha na ufadhili au uratibu wa machafuko ya kisiasa nchini Kenya, huku likielezea madai hayo kama yasiyokuwa na msingi.

“Uwazi na utaratibu wa haki ni muhimu katika jamii za kidemokrasia,” shirika hilo lilisema, na kuongeza kuwa limefanya kazi nchini Kenya tangu 2005 na limefuata sheria za nchi wakati likisaidia ushirikishwaji  wa raia, utawala wa uwajibikaji na kazi za sera katika maeneo kama vile mageuzi ya kiuchumi na mabadiliko ya tabia nchi.

Dhuluma aliyopata Kagoro sio ya kwanza Kenya. Kwa zaidi ya mwaka sasa, wanaharakati katika ukanda wa Afrika Mashariki wamenyanyaswa, kufurushwa, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu katika mazingira ambayo yamekera mashirika hayo.

Mwezi Januari 2025, mwanaharakati wa kitanzania Maria Sarungi Tsehai alitekwa Nairobi na wanaume wenye bunduki kabla ya kuachiwa kufuatia shinikizo la umma. Alisema aliamini uanaharakati wake ulimfanya kuwa mhathiriwa lakini aliahidi kutokoma kupigania mageuzi ya kidemokrasia.

Activists

Miezi michache baadaye, mwanaharakati wa kenya Mwabili Mwagodi alipotea nchini Tanzania katika mazingira tata kabla ya kupatikana akiwa ameachwa katika kaunti ya Kwale. Baadaye alidai kupewa mateso wakati akiwa kizuizini.

Februari 2026, alikamatwa tena katika mpaka wa Lunga Lunga na kushtakiwa na makosa kuchapisha habari za uongo. Aliachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea. Wanaharakati wa kenya Bob Njagi na Nicholas Oyoo pia wanadaiwa kutekwa Uganda wakati wa kampeni za upinzani na baadaye kuwekwa kizuizini kwa siku 38 katika kituo cha kizuizini cha siri.

Hivi karibuni, Februari 2026, mwanaharakati wa kitanzania Mshabaha Hamza alitekwa nchini Kenya lakini akaokolewa kabla kuvukishwa mpaka kuelekea Tanzania, kwa mujibu wa Amnesty International.

Zaidi ya wanaharakati, viongozi wengine maarufu wa upinzani katika ukanda wa Afrika Mashariki pia wamenyanyaswa na kunyimwa haki zao za kimsingi.

Nchini Uganda, kiongozi wa zamani wa upinzani Dr. Kizza Besigye bado anashikiliwa miezi michache baada ya kukatwa mwishoni mwa 2024. Kukamatwa kwake kumekosolewa na kupingwa vikali na mashirika ya haki za binadamu wanaodai makosa anayokisiwa kufanya ni ya kubandikizwa.

Nchini Tanzania, kiongozi wa upinzani Tundu Lissu bado anapambana  kesi za kisheria ambazo zimemzuia kushiriki vikamilifu katika siasa. Ingawa amepinga kesi dhidi yake, hatma yake bado Haijulikani, huku wafuasi wake wakisema kuwa kesi hizo zimeendelea na kuathiri kazi yake kuwasemea kisiasa wananchi wanyonge. Mashirika ya haki ya kibinadamu yamesema kwamba unyanyasaji wa wanaharakati na viongozi wa upinzani unadhihirisha wasiwasi mpana kuhusu uhuru wa kujieleza na nafasi ya kiraia katika ukanda huu.

Open Society imesisitiza kwamba haifadhili wala kuandaa maandamano ya kisiasa na kwamba kazi yake inasaidia kuwaelimisha wananchi juu ya haki zao. Shirika hilo limesema linatafuta ufafanuzi rasmi kutoka kwa mamlaka ya Kenya kuhusiana na kwa nini lilimfurisha Kagoro.

Kenya imekuwa ikionekana kama eneo salama kwa wanaharakati na watetezi wa haki za kibinadamu katika ukanda wa afrika mashariki. Hata hivyo, matukio ya hivi karibuni yameibua maswali kuhusu kama nafasi hiyo inazidi kupungua. Uchunguzi unapoendelea katika kesi hizo, mashirika ya kiraia yamesema yataendelea kudai uwazi na uwajibikaji, huku yakionya kwamba ulinzi wa wanaharakati ni muhimu katika kulinda demokrasia.