Masuala manne ya kufahamu kuhusu Kesi ya uchaguzi Kenya

Majaji saba wa Mahakama ya Upeo Kenya.

Mahakama ya upeo siku ya ijumaa ilikamilisha zoezi la siku tatu la kusikiza pande zote katika kesi inayopinga matokeo ya uchaguzi wa agosti tisa, uchaguzi ambao naibu wa rais William Ruto alitangazwa kuwa mshindi na tume ya uchaguzi nchini Kenya (IEBC)

Mpinzani wake mkuu Raila Odinga mwenye umri wa miaka 77 alipoteza nafasi yake ya tano ya kuwa kiongozi wa taifa hilo, na akasisitiza kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu na kudai kuwa ako na ushaidi tosha kuonyesha ulimwengu jinsi matokeo yalibadilishwa kwa faida ya William Ruto.

Majaji saba wa mahakama hiyo wakiongozwa na Martha Koome wanatarajiwa kutoa uamuzi wao siku ya jumatatu tarehe 5 Septemba ambayo ndio siku ya mwisho kisheria.

Kesi hii iliwasilishwa mahakamani baada ya tume ya uchaguzi na mipaka IEBC kumtangaza William Ruto mwenye umri wa miaka 55 kama rais mteule tarehe 15 agosti.

Odinga akipoteza kwa kura 230,000 hata ingawa aliungwa mkono na rais anayestaafu Uhuru Kenyatta pamoja na chama chake cha Jubilee.

Waziri huyo wa zamani alipinga matokeo hayo na kuilaumu IEBC kwa kuvuruga uchaguzi huo.

Hata hivyo si mara ya kwanza anafanya hivyo, kiongozi huyo wa chungwa alipinga matokeo ya mwaka 2013 na 2017 mahakamani.

Agosti mwaka wa 2017 mahakama ya upeo chini ya uongozi wa jaji mkuu mstaafu David Maraga ilibatilisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta baada ya Odinga kuwasilisha kes katika mahakama hiyo.

Tume ya IEBC imekuwa inashinikizwa kuandaa uchaguzi wa uwazi, huru na haki baada ya mahakama kufuta ushindi wa rais Kenyatta mwaka wa 2017.

Baada ya IEBC kutangaza matokeo ya uchaguzi wa mwaka wa 2022, kesi saba zilizowasilishwa mahakamani ambazo viliunganishwa na kuwa moja zote zikidai kulishuhudiwa makosa chungu nzima katika uchaguzi huu uliokamilika.

Kesi ya Odinga lenye kurasa 72 inadai kuwa wadukuzi waliingia kwenye sava za IEBC na kubadilisha matokeo kwenye fomu zilizotumika kuwasilisha matokeo kitoka kwenye vituo vya kupigia kura hadi kwenye kituo cha kitaifa cha kujumuisha matokeo ya urais.


Odinga pia anadai kuwa William Ruto hakufikisha asilimia 50+kura 1 ya kura zote zilizopigwa.

Jaji mkuu Martha Koome, alisema wameorodhesha masuala tisa ambayo watatumia kufikia uamuzi wao wa mwisho katika kesi hiyo.

Majaji hao watajaribu kubaini iwapo tovuti ya iebc ilidukuliwa na iwapo fomu za kusambaza matokeo ziliitilafiwa.

Pia watahakiki mfumo wa kidigitali wa IEBC kuona ikiwa masuala yaliopeleka uchaguzi wa 2017 kubatishiwa yalizingatiwa mwaka huu au la.

Swali ambalo wengi wanajiuliza ni je, majaji wanawezi kutoa uamuzi wa aina gani?

Iwapo mahakama itapata makosa ambayo yanaweza kuwa yaliathiri matoke yaliotangazwa na IEBC,inaweza kuvunjilia mbali uchaguzi huo na wakenya kurejea debeni baada ya siku 60.

Mahakama vilevile inaweza kukosoa mchakato wa uchaguzi huo na kusema makosa yaliofanyika hayafai kupelekea uchaguzi huo kubatilishwa.

Lakini iwapo itapatikana kuwa rais mteule hakufikisha asilimia 50 na kura moja jinsi katiba ya Kenya inasema, itaagiza marudio ya uchaguzi ndani ya siku 30.

Na mwisho inaweza kuidhinisha kuchaguliwa kwa William Ruto kama rais mteule na kupisha uapisho wake kufanyika septemba 13.

Hata hivyo uamuzi wa mahakama ya upeo utaafikiwa na jinsi wengi wa majaji wataamua katika kesi hiyo.

Mahakama ya upeo ndio mahakama ya juu zaidi nchini Kenya na uamuzi wake ndio wa mwisho.