Mahakama ya upeo ya Kenya leo jumanne imeanza kikao cha kwanza cha kutathmini masuala yatakayoshughulikiwa katika kesi zilizowalishwa kupinga kutangazwa kwa rais mteule William Ruto kama mshindi wa uchaguzi wa agosti.
Mahakama hiyo chini ya uongozi wa jaji mkuu Martha Koome imeorodhesha masuala 9 ambayo itakuwa inafanya uamuzi kuyahusu baada ya kukujumuisha baadhi ya kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
Masuala hayo ni,
- Iwapo teknolojia iliyotumika na Tume ya uchaguzi na mipaka IEBC katika uchaguzi iliafikia viwango vya ubora wa kuwezesha uchaguzi unaoweza kuthibithitishwa na ulio salama kwa lengo la kutoa matokeo sahihi.
- Iwapo kulikuwa na visa vya kuitilafiana na fomu ya 34A zilizowasilishwa na zilizopakuliwa katika tovuti ya IEBC.
- Iwapo kulikuwa na tofauti kati ya fomu 34A zilizopakuliwa katika tovuti ya IEBC, zilizowasilishwa katika kituo cha kitaifa cha kujumisha matokeo na zilizopewa mawakala katika vituo vya kupigia kura.
- Iwapo kuahirishwa kwa chaguzi za ugavana kaunti za Kakamega na Mombasa na maeneo bunge manne pamoja na wadi mbili ilipangwa ili kupunguza idadi ya wapiga kura waliojitokeza kupiga kura na kuaathiri mgombea wa Azimio Raila Odinga ambaye ndiye mlalamishi mkuu.
- Iwapo kulikuwa na tofauti zisizoelezeka kati ya kura za urais na za nyadhifa nyingine zilizopingwa siku ya uchaguzi.
- Iwapo Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ilifanya uthibitisho wa kutosha, ujumuishaji na kwa mujibu wa kipengee cha 138 (3) c na 138 (10) ya katiba.
- Iwapo rais mteule wa taifa la Kenya William Ruto alipata asilimia 50+1 ya kura zote zilizopigwa kulingana na kipengee cha 138 (4) cha katiba ili kutangazwa mshindi.
- Iwapo kulikuwa na makosa katika idadi ya kura na kuathiri matokeo ya mwisho ya uchaguzi yaliotangazwa na IEBC.
- Maelekezo ambayo mahakama ya juu zaidi inaweza kutoa kuhusu kesi hizo za urais.