Mataifa 15 ya pekee ya Afrika yamechanja kikamilifu 10% ya watu wao dhidi ya UVIKO 19.

Mataifa 15 ya Africa, ikiwa thuluthi moja ya mataifa 54 ya bara Afrika yamechanja kikamilifu 10% ya watu wao dhidi ya UVIKO 19.

Lengo la kimataifa la kuwachanja 10% ya idadi ya watu katika mataifa ya bara Afrika kufikia Septemba 30 liliwekwa mwezi Mei na Shirika la Afya Duniani (WHO). Takriban 90% ya mataifa yenye uwezo zaidi duniani yamefikia lengo la WHO.

Visiwa vya Ushelisheli na Mauritius vimefaulu kuchanja asilimia 60 ya watu wake kulingana na data za WHO. Morocco imefaulu kuchanja 48% ya watu wake na Tunisia, Comoros na Cape Verde wamechanja zaidi ya 20% ya watu wake.

Mataifa mengi ya Afrika yaliyofikia malengo ya kuchanja watu wake ni yale yenye idadi ndogo ya watu ikiwa ni mataifa ya visiwa yanayoendelea.

Mataifa haya yamefaidika kwa kupata dozi za kutosha za kuwachanja watu wake ikiwa ni misaada kutoka mataifa tofauti wakiongeza na chanjo kutoka mpango wa COVAX, jukwaa la ulimwengu la kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo. Nusu ya mataifa 52 ya Afrika yamepokea chanjo na kuchanja kikamilifu 2% pekee ya raia wake.

“Data ya hivi punde inaonesha kuna ongezeko la idadi ya watu waliochanjwa ingawa kuna safari ndefu kuelekea kuchanja 40% ya watu wake kufikia mwishoni mwa mwaka huu.” Dkt. Richard Mihigo, Mratibu wa chanjo barani Afrika kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dkt. Richard Mihigo WHO

Mataifa tisa kutoka Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Morocco na Tunisia yamefikia malengo ya kuchanja 10% ya watu wake kufikia mwanzo wa mwezi Septemba na mataifa mengine sita yakielekea kufikia lengo hilo kutokana na ongezeko la upatikanaji wa chanjo.

Jumla ya chanjo milioni 23 zimewasili Afrika mwezi Septemba, ikiwa ni ongezeko mara 10 ikitofautishwa na mwezi Juni. Hata hivyo Waafrika milioni 60 pekee wamechanjwa kikamilifu na 2% ya chanjo bilioni 6 zilizotolewa kote duniani zimetumika barani Afrika.

COVAX inashirikiana na wafadhili kutambua mataifa ambayo yanauhitaji mkubwa wa chanjo na kuwatumia na kuboresha upatikanaji wa chanjo kutoka kwa wafadhili zaidi.

Visa vipya vya UVIKO 19 vimepungua barani Afrika kwa 35% hadi visa 74,000 katika wiki ya mwisho ya mwezi Septemba. Takriban vifo 1800 viliripotiwa katika mataifa 34 katika kipindi hicho. Kirusi cha Delta kimepatikana katika mataifa 39 Afrika. Kirusi cha Alpha kimepatikana katika mataifa 45 na kirusi cha Beta katika mataifa 40.

“Licha ya kuwa visa vya maambukizi vinapungua lazime tuwe waangalifu na tuendelee kuzingatia usafi ili kuepuka maambukizi mapya,kuvaa barakoa,kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka mikusanyiko ya watu wengi.” Dkt. Richard Mihigo, Mratibu wa chanjo barani Afrika kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).