Uingereza inasitisha safari zote za ndege kutoka Afrika Kusini na nchi nyingine tano katika eneo hilo ili kukabiliana na ugunduzi wa kirusi kipya kinachoambukiza na kuenea kwa haraka.
Kuanzia adhuhuri siku ya Ijumaa, safari za ndege za moja kwa moja kutoka Afrika Kusini, Namibia, Botswana, Zimbabwe, Lesotho na Eswatini zitasitishwa hadi ilani nyingine itakapotolewa.
Akitangaza vizuizi hivyo, waziri wa afya wa Uingereza, Sajid Javid, alisema inawezekana kwamba chanjo za sasa zinaweza kuwa na ufanisi mdogo dhidi ya kirusi hicho kinachobadilika kwa haraka.
Hakuna visa vyovyote ambavyo vimegunduliwa nchini Uingereza,ila ripoti zinasema kuwa watu 59 walioambukizwa kirusi hicho wamegunduliwa nchini Afrika Kusini , Hong Kong na Botswana.
Wataalamu wa Afrika Kusini wanasema kirusi hicho kwa jina la kisayansi B.1.1.529, kilikuwa kimeenea kwa kasi miongoni mwa wanafunzi mjini Pretoria na kuwa ni kirusi hatari zaidi kuwahi kuonekana kufikia sasa na kuna wasiwasi kwamba kina uwezo wa kukwepa kinga.
Wataalam kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni wanatarajiwa kukutana na maafisa wa Afya wa Afrika Kusini siku ya Ijumaa 26 Novemba.
Singapore na mataifa mengine ya Ulaya ikiwemo Ujerumani pia yamepiga marufuku safari kutoka Afrika Kusini ili kusitisha kuenea kwa kirusi kipya cha UVIKO 19, tangazo hili lilitolewa na kaimu Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn siku ya Ijumaa.
Sheria hizo mpya, zitaanza kutekelezwa Ijumaa usiku na zitaathiri Afrika Kusini na “pengine mataifa jirani” Spahn alisema, huku raia wa Ujerumani pekee wakiruhusiwa kuingia nchini humo.
Ila ni lazima wakae kwenye karantini kwa siku 14 baada ya kuwasili hata kama wamechanjwa. “Jambo la mwisho tunalohitaji sasa ni lahaja mpya iliyoletwa ambayo husababisha shida zaidi,” Spahn alisema.