Maafisa wa polisi wameutambua mwili wa mwanaume uliopatikana umeingizwa ndani ya sanduku la chuma kando ya barabara ya Kipkenyo-Kaptinga katika kaunti ya Uasin Gishu kama ya mwanaharakati wa mahusiano ya jinisa moja (LGBTQ) Edwin Chiloba.
Mwili wa marehemu uligunduliwa baada ya wahudumu wa bodaboda waliokuwa wakiendelea na shughuli zao katika eno hilo, kuwafahamisha polisi kuhusu gari walilolitilia shaka ambalo lilikuwa limetupa sanduku la chuma kando ya njia.
Kulingana na walioshuhudia kisa hicho numbari ya usajili ya gari hilo lilikuwa limebanwa.
Baada ya kufika katika eneo hilo, polisi walifungua sanduku hilo na kubaini mwili wa Chiloba ambao ulikuwa umeanza kuoza ukiwa umevalishwa nguo za mwanamke.
Kwa sasa mwili huo umesafirishwa katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi Eldoret kwa ukaguzi ili kubaini chanzo cha kifo chake.
Maafisa wa polisi pia wameanzisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo ya kikatili huku wanachama wa jumuiya ya LGBTQ nchini Kenya wakimuomboleza mwanaharakati huyo.
Mwaka uliopita, Chiloba alinusurika shambulizi lililotekelezwa na watu wasiojulikana ambao walimshambulia hadharani na kumuacha na majeraha mabaya usoni.
Ikizungumzia mauaji hayo, Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KHRC) imetaja kuongezeka kwa unyanyasaji dhidi ya jamii ya LGBTQ kuwa jambo la kutisha.
Kauli ya KHRC imeungwa mkono na wadau mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii akiwemo Katibu mkuu wa shirikisho la wateja nchini Kenya Stephen Mutoro, ambaye amelaani mauaji hayo ya kinyama.
Ingawa mahusiano ya watu wa jinsia moja yamesalia kuwa haramu nchini Kenya, mahakama za nchi hiyo zimethibitisha haki zilizohakikishwa chini ya kifungu cha 28 na 31.