Baraza la mawaziri la Uganda ambalo hukutana kila Jumatatu na kuongozwa na rais, limeazimia kuanza kupata masomo ya Kiswahili kwa saa chache asubuhi kwa mwaka mmoja ujao.
Hayo ni kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu wa kwanza wa nchi hiyo na Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Rebecca Kadaga.
Kadaga ambaye alikuwa akifungua kongamano la pili la kila mwaka la Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) jijini Kampala, alisema hatua hiyo itawawezesha wanachama kuanza kufanya mikutano kwa lugha ya Kiswahili.
Mnamo Julai 2022, Baraza la Mawaziri la Serikali ya Uganda lilipitisha na kuidhinisha Kiswahili kama lugha rasmi ya nchi na kupendekeza kuwa lugha hiyo iwe ya lazima kufundishwa na kuchunguzwa katika Shule za Msingi na Sekondari.
Kadaga aliuambia mkutano huo kuwa Uganda inafurahi kuandaa mkutano huo pamoja na vikao vijavyo vya mahakama vitakavyofanyika mjini Kampala mwezi ujao.
Alizipongeza nchi wanachama wa EAC kwa kuongeza mamlaka ya EACJ kujumuisha masuala yanayohusu usuluhishi wa umoja wa forodha.
Majaji wakuu, majaji na watendaji wa sheria kutoka mataifa ya EAC wanahudhuria mkutano huo utakaofungwa na Rais Yoweri Museveni siku ya Ijumaa.