Mawaziri wapya Mutahi Kagwe, Lee Kinyanjui na William Kabogo Ijumaa wameapishwa kuanza kazi, saa chache baada ya kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Watatu hao wameapishwa katika hafla hiyo ilishuhudiwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Kagwe ni waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo, Kabogo ni waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi Dijtali ilhali Kinyanjui ni waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda.
Waliidhinishwa na Bunge la Kitaifa Alhamisi katika kikao maalum kilichoitishwa na Spika Moses Wetang’ula.
Watatu hao sasa wamechukua nafasi za Andrew Karanja, Margret Nyambura na Salim Mvurya ambaye alitumwa tena katika Wizara ya Michezo.
Karanja pia aliidhinishwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Brazil, huku Nyambura akikataa uteuzi wa kuhudumu kama Balozi wa Kenya nchini Ghana.