Viongozi tisa wa mataifa ya Afrika wahudhuria kikao cha Jumatatu cha ufunguzi wa mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ya COP15 ya kupambana na kuenea kwa jangwa na uharibifu wa ardhi ambayo yameharibu maeneo makubwa ya bara hilo huku kukiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa (UNCCD), nchi 196 pamoja na Umoja wa Ulaya — unakutana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu, mjini Abidjan.
Miongo kadhaa ya kilimo kisicho endelevu kimedhoofisha udongo duniani kote na kuharakisha ongezeko la joto duniani na upotevu wa viumbe, UNCCD inasema, huku takriban asilimia 40 ya ardhi ikiharibika kote duniani.
“Mkutano wetu wa kilele unafanyika katika muktadha wa dharura ya hali ya hewa ambayo inaathiri vibaya sera zetu za usimamizi wa ardhi na kuzidisha ukame,” Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara alitangaza.
“Watu wetu waliweka matumaini makubwa kwetu, hatuna haki ya kuwakatisha tamaa.”
“Tuchukue hatua haraka, tuchukue hatua kwa pamoja ili kuyapa maisha mapya ardhi yetu,” alihimiza.
Muhammadu Buhari wa Nigeria, Mohamed Bazoum wa Niger na Felix Tshisekedi wa DR Congo walikuwa miongoni mwa viongozi wa bara hilo wakimsikiliza mwenyeji wao Rais wa Ivory Coast.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa akihutubia mkutano huo kwa njia ya video.
Ouattara aliwasilisha Abidjan Initiative kukusanya dola bilioni 1.5 katika kipindi cha miaka mitano kurejesha “mifumo ya mazingira ya misitu iliyoharibiwa” ya Ivory Coast na kukuza usimamizi endelevu wa udongo.
Ivory Coast ni miongoni mwa mataifa mengi ya Afrika yaliyoathiriwa vibaya na hali ya jangwa.
Misitu imepungua kwa asilimia 80 tangu 1900 — kutoka hekta milioni 16 hadi milioni 2.9 mwaka jana.
“Kwa kiwango cha sasa, misitu yetu inaweza kutoweka kabisa ifikapo 2050,” Ouattara alionya.
COP15 itaendelea hadi Mei 20 na inatazamiwa kusikiliza mapendekezo mapya ya kujaribu kusitisha kuenea kwa hali ya jangwa na kuzorota kwa ubora wa ardhi.
Mkutano huo utatilia maanani hasa urejeshaji wa hekta bilioni moja za ardhi iliyoharibiwa ifikapo mwaka 2030, matumizi ya ardhi yanayoweza kudhibitisha siku za usoni na kustahimili ukame, UNCCD ilisema.
Mjadala unatarajiwa kujumuisha swali la mpango wa “Great Green Wall” kurejesha hekta milioni 100 za ardhi kame kutoka Senegal magharibi mwa Afrika hadi Djibouti katika mashariki mwa Afrika kufikia 2030.