Salwan Momika, mchomaji wa Kuran na mkimbizi kutoka Iraq, ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake huko Södertälje, karibu na Stockholm, Uswidi.
Kulingana na ripoti Momika alikuwa akifanya matangazo ya moja kwa moja wakati wa tukio hilo. Polisi walifika nyumbani kwake na kusitisha matangazo hayo.
Tayari watu watano wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo, huku uchunguzi wa mauaji hayo ukiendelea.
SALWAN MOMIKA NI NANI?
Salwan Momika alikuwa mkimbizi kutoka Iraq na mwanaharakati anayejulikana kwa maandamano yake ya kuchoma Kuran nchini Sweden.
Alizaliwa tarehe 23 Juni 1986 katika mji wa Qaraqosh, mkoa wa Nineveh, Iraq, katikafamilia ya Kikristo ya Assyrian Catholic.
Wakati wa vita vya kimadhehebu kati ya mwaka 2006 na 2008, alijiunga na Chama cha Wazalendo wa Assyria na kufanya kazi kama mlinzi wa usalama katika makao makuu ya chama hicho huko Mosul.
Momika alikuwa mwanachama wa milisia ya Kikristo na alihusika katika vita dhidi ya kundi la Islamic State (ISIS) kabla ya kuhamia Sweden mwaka 2018 baada ya kukimbia mzozo wa madaraka na kiongozi mwingine wa kundi la wanamgambo wa Kikristo.
Momika alipata umaarufu kwa kuchoma na kudhalilisha Kuran hadharani, vitendo ambavyo vilisababisha hasira na maandamano katika nchi nyingi za Waislamu.
Alitetea maandamano yake kama njia ya kupinga dini ya Uislamu, akisema kuwa alitaka kulinda raia wa Sweden kutokana na ujumbe wa Kuran.
Kwa bahati mbaya, Momika aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake huko Södertälje, karibu na Stockholm, wakati akifanya matangazo ya moja kwa moja. Polisi wamewakamata watu watano kuhusiana na tukio hilo, na uchunguzi wa mauaji unaendelea