Mwanajeshi wa Burkina Faso Paul-Henri Sandaogo Damiba siku ya Alhamisi alimteua mwanauchumi Albert Ouedraogo kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Ouedraogo mwenye umri wa miaka 53, ambaye uteuzi wake ulikuja kwa amri iliyotiwa saini na Rais Damiba, ameongoza kampuni ya ushauri na ukaguzi wa hesabu tangu 2007.
“Waziri mkuu mpya ana uzoefu mkubwa katika uwanja wa usimamizi wa utawala wa umma, miradi ya maendeleo na makampuni ya kibinafsi.”ofisi ya Damiba ilisema.
Damiba, Luteni Kanali mwenye umri wa miaka 41, alichukua mamlaka mnamo Januari 24, na kumuondoa rais mteule Roch Marc Christian Kabore.
Aliapishwa kama rais na mkuu wa vikosi vya jeshi na baraza kuu la kikatiba mnamo Februari 16. Sherehe fupi za kurasimisha nafasi yake zilifanyika Jumatano.
Siku ya Jumanne, Damiba alitia saini kinachojulikana kama katiba ya mpito ambayo ilitangaza uchaguzi utafanyika miezi 36 baada ya kuapishwa kwake.
Muda huo ulikuwa mrefu zaidi ya ile miezi 30 ambayo ilikuwa imependekezwa na tume iliyoundwa na jeshi.
Mkataba huo unaeleza kuwa rais hastahili “kushiriki uchaguzi wa urais, ubunge na manispaa ambao utaandaliwa ili kukomesha kipindi cha mpito.”
Bunge la wabunge 71 na serikali ya watu 25 inayoongozwa na waziri mkuu zinaundwa ili kuhakikisha mabadiliko hayo.
Wanachama wao pia watazuiwa kugombea kura baada ya mpito.
Siku ya Jumatano mkuu wa nchi aliagiza ukaguzi wa jumla wa sekta ya umma, hatua inayolenga kukuza utawala bora.
Moja ya nchi masikini zaidi duniani, taifa hilo lina historia ndefu ya hali tete tangu kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.