Mchungaji wa Kenya afikishwa mahakamani kwa mauaji ya kidini

Mwinjilisti tajiri na mashuhuri Ezekiel Odero mkuu wa ‘New Life Prayer Center and Church’. (Picha na SIMON MAINA / AFP)

Mchungaji mmoja maarufu nchini Kenya anakabiliwa na kesi ya mahakama siku ya Alhamisi kuhusiana na ugunduzi wa kutisha mwezi uliopita wa makumi ya maiti kwenye makaburi ya halaiki.

Ezekiel Odero, mwinjilisti tajiri anayejivunia ufuasi mkubwa, anachunguzwa kwa msururu wa mashtaka yakiwemo mauaji, kusaidia kujiua, utekaji nyara, itikadi kali, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, ulaghai na utakatishaji fedha.
Waendesha mashtaka wanamshutumu Odero kwa uhusiano na kiongozi wa madhehebu Paul Nthenge Mackenzie, ambaye yuko kizuizini akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi kutokana na vifo vya zaidi ya watu 100 wengi wao wakiwa watoto.
Mackenzie, mkuu wa kanisa la Good News International Church, anadaiwa kuwachochea wafuasi wake kufa njaa ili “kumlaki Yesu” katika kisa ambacho kimewashangaza sana Wakenya.
Odero alifika mahakamani katika jiji la Mombasa kabla ya kusikilizwa kwa kesi hiyo, huku wafuasi wapatao 50 wakikusanyika nje, wengine wakiwa wamevalia mavazi meupe, wengine nyekundu, na kusali wakiwa na biblia mkononi.
Polisi wa Kenya walikuwa wamemkamata Odero Alhamisi iliyopita kutokana na “mauaji mengi ya wafuasi wake” na kufunga Kituo chake cha New Life Prayer Centre and Church lililoko kusini mwa mji wa pwani wa Malindi.
Jumla ya watu 109 hadi sasa wamethibitishwa kufariki katika kile kilichopewa jina la “mauaji ya msitu wa Shakahola”.

Uchunguzi wa miili 40 kati ya miili iliyofukuliwa msituni kutoka Malindi hadi sasa uligundua kuwa huku njaa ikionekana kuwa chanzo kikuu cha vifo, baadhi ya wahasiriwa walinyongwa, kupigwa au kuzidiwa.

Waendesha mashtaka wanasema wana habari za kuaminika zinazohusisha maiti zilizofukuliwa huko Shakahola na vifo vya “wafuasi wasio na hatia” kadhaa wa Odero.

Waendesha mashtaka wamesema katika nyaraka za mahakama kwamba Odero na Mackenzie wanashiriki “historia ya uwekezaji wa biashara” ikiwa ni pamoja na kituo cha televisheni kilichotumiwa kupitisha “ujumbe mkali” kwa wafuasi.

Katika kesi aliyowasilisha mahakamani mapema wiki hii, Odero alisema alitaka “kujitenga sana” na Mackenzie na hakukubaliana na mafundisho yake.

Cliff Ombeta, mmoja wa mawakili wa Odero, alikuwa amewaambia wanahabari katika kikao cha mahakama cha Jumanne kwamba hakuna ushahidi wa kumuunganisha pasta na uvumbuzi wa Shakahola.
“Ushahidi lazima uletwe. Ni kesi ambayo lazima uthibitishe,” alisema.

Nchi hiyo yenye Wakristo wengi wa kidini imepigwa na butwaa na kisa hicho na Rais William Ruto ameahidi kuchukua hatua dhidi ya makanisa na dhehebu potovu ambazo zimejiingiza katika uhalifu.