Mapinduzi ya serikali ya Guinea yaliongozwa na mkuu wa vikosi
maalum Mamady Doumbouya, ila Mamady Doumbouya ni
nani haswa?
Luteni Kanali Doumbouya ametoka jamii ya Malinke sawa
na Rais Alpha Conde, jamii ya Malinke inapatikana maeneo
ya Kankan katika mpaka wa Côte d’Ivoire na Mali.
Kiongozi huyu wa mapinduzi nchini Guinea, alihitimu katika
mafunzo ya kijeshi kutoka Chuo cha Ecole Guerre nchini
Ufaransa na alikuwa kwenye Jeshi la Foreign Legion, ambako
alifanya vyema hadi akapandishwa cheo kuwa Master corporal.
Akiwa mwanajeshi, ameshiriki operesheni nchini Afghanistan na
katika nchi tofauti Afrika.
Luteni Kanali Doumbouya ni mtaalam katika usimamizi wa ulinzi,
amri na mkakati na amepata mafunzo ya kitaalam Israeli, Senegal
na Gabon.
Mamady Doumbouya mwenye umri wa miaka 41 alianza
kujulikana kwa watu wa Guinea mwaka wa 2018 aliposhiriki
gwaride la kijeshi katika sherehe za miaka 60 za uhuru wa nchi.
Alichaguliwa kuwa mkuu wa kikosi kipya cha majeshi
kilichoundwa cha SFG, chenye majukumu ya kupambana na
ugaidi na uharamia wa baharini. Wanajeshi wa kikosi hiki huvalia
kofia nyekundu, miwani ya jua na sare za kuvutia.
Matatizo ya Luteni Kanali na uongozi wa nchi unasemekana
kuanza alipozuiliwa kuondoa kikosi cha SFG chini ya Wizara ya
Ulinzi.
Siku ya Jumapili 5 Septemba, Luteni Kanali Mamady Doumbouya,
akiwa amejifinika bendera ya Guinea alitangaza mapinduzi ya
serikali na kukamatwa kwa Rais wa Guinea Alpha conde na
kufutwa kwa katiba ya nchi.Nafasi za viongozi wa kisiasa wa
mikoa zikachukuliwa na makamanda wa jeshi, na mawaziri wote
wakahitajika kuhudhuria mkutano Jumatatu.
Katika mahojiano na vituo vya habari, Luteni Kanali Doumbouya,
alisema aliongoza mapinduzi hayo ili kuiokoa nchi yake kutoka
kwa ufisadi, umasikini na rushwa uliokuwa umekithiri chini ya uongozi wa Rais Conde.
Mamady Doumbouya, ameahidi kuunda serikali ya umoja katika
wiki chache zijazo na kufunguliwa kwa mipaka ya nchi na ya
anga.