John Wagesa Heche ndiye makamu mwenyekiti mpya wa Chama cha Demeokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Alichaguliwa tarehe 22 Januari mwaka wa 2025 baada ya kumshinda mpizani wake wa karibu Ezekia Wenje. Heche alipata kura 577 ambayo ni asilimia 57 kisha Wenje akapata kura 372 sawa na asilimia 37 za kura zote zilizopigwa.
John Wagesa Heche alizaliwa Julai 14, 1981 Tarime, Mkoani Mara. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Bulima, kisha kujiunga na Shule ya Sekondari ya Musoma Alliance ambapo alihitimu kidato cha nne mwaka 1997
Baada ya hapo, alijiunga na Bunda Teachers’ Training College na kupata diploma ya ualimu mwaka 2004. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (St. Augustine University of Tanzania-SUAT) na kuhitimu shahada ya ualimu mwaka 2009
Katika ulingo wa siasa, Heche alichaguliwa kuwa Diwani wa halmashauri ya wilaya ya Tarime mjini mwaka wa 2010 kabla ya kuwa mbunge wa Tarime Vijijini mwaka 2015. Alichaguliwa kuwa mbunge akiwa na umri wa miaka 34. Alihudumu katika Bunge la 11 la Tanzania kuanzia Oktoba 29, 2015 hadi 2020
Heche vile vile amehudumu katika ngazi mbali mbali za chama ambapo alikuwa Kiongozi wa baraza la vijana Chadema, Bavicha taifa, Mwnyekiti wa Kanda ya Serengeti na vile vile mjumbe wa kamati kuu ya chama.
Punde tu baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi ya umakamu mwenyekiti, Heche amesema malengo makuu ya yake na chama ni kushinda uchaguzi wa 2025 kwa kuondoa CCM (Chama cha Mapinduzi) madarakani, na kutumia rasilimali za Tanzania kunufaisha Maisha ya wananchi.
Heche anachukua nafasi aliyokuwa akishikilia Tundu Lissu ambaye sasa ndiye mwenyekiti wa Chadema baada ya kumshinda Freeman Mbowe kwenye uchaguzi uliyofanyika tarehe 22 Januari 2025.
John Heche ana umri wa miaka 43