Mfahamu zaidi rais wa mwisho mweupe wa Afrika Kusini FW de Klerk

FW de Klerk, Rais wa zamani wa Afrika Kusini

Frederik Willem de Klerk rais wa mwisho mzungu wa Afrika Kusini aliaga dunia Alhamis 11 Novemba 2021 akiwa na umri wa miaka 85.

FW de Klerk, alizaliwa mjini Johannesburg tarehe 18 Machi 1936 alikuwa mwanasiasa na mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel. Alihudumu kama rais wa Afrika Kusini kutoka 1989 hadi 1994 na naibu wa rais kutoka 1994 hadi 1996 baada ya uchaguzi wa kwanza uliowajumusiha waafrika Kusini wote ambapo Nelson Mandela aliibuka mshindi na kuwa rais wa kwanza mweusi nchini humo.

Kabla kuwa rais wa Afrika Kusini,De Klerk alihudumu kama waziri akiwa katika chama cha National Party kilichoongozwa na P. W. Botha.

Katika wadhfa wake kama waziri aliunga mkono na kutekeleza ubaguzi wa rangi ambao uliwapendelea waafrika kusini weupe.Baada ya kujiuzulu kwa Botha mwaka wa 1989, de Klerk alichukua nafasi yake kama kiongozi wa chama cha National Party na baadae kama rais wa nchi.

De Klerk alifahamu fika kuwa ongezeka la uhasama wa kikabila na ghasia kungeisababishia Afrika Kusini kuzama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na vya rangi. Katika mapigano hayo vikosi vya usalama vya serikali vilitekeleza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kuhimiza mapigano kati ya makabila ya Xhosa na Zulu. De Klerk baadae alikanusha kuidhinisha kwa mapigano hayo, alliruhusu maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi kufanyika, alihalalisha aina mbalimbali za vyama vya siasa vilivyopigwa marufuku hapo awali na kuwaachilia huru wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi, ikiwemo Nelson Mandela.

FW de Klerk na Nelson Mandela

Vitendo vyake vilisaidia kukomesha enzi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, na akawa mmoja wa manaibu marais wawili baada ya uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1994 ambao ulishuhudia Bw Mandela akiwa rais. Mwaka wa 1993 aliomba radhi hadharani  kwa madhara ya ubaguzi wa rangi na wala sio ubaguzi wa rangi wenyewe. Katika nafasi yake kama makamu wa rais, aliunga mkono sera za serikali huria za uchumi lakini alipinga Tume ya Ukweli na Maridhiano iliyoundwa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu kwa sababu alitaka msamaha kamili kwa uhalifu wa kisiasa.

FW de Klerk na Nelson Mandela walishinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa pamoja mnamo 1993. Ijapokuwa uhusiano kati ya De Klerk na Mandela mara nyingi ulijaa mizozo mikali,  alimtaja Mandela kama mtu mwadilifu sana.

Nelson Mandela na FW de Klerk baada ya kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel

Nelson Mandela alipofariki mwaka 2013, De Klerk alitoa heshima kwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo. “Alikuwa muunganishi mkuu na mtu wa pekee sana katika suala hili, zaidi ya yote aliyofanya. Msisitizo huu wa upatanisho ulikuwa urithi wake mkubwa.”