Mfalme Philippe wa Ubelgiji aliwasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumanne, katika ziara ya kihistoria katika nchi hiyo ya Afrika ya kati ambayo babu yake aliwahi kutawala kikatili.
Mfalme huyo atafanya ziara ya siku sita inadaiwa kuwa nafasi ya maridhiano baada ya ukatili uliofanywa chini ya utawala wa kikoloni wa Ubelgiji.
Ziara hiyo inajiri miaka miwili baada ya Philippe kumwandikia Rais wa Congo Felix Tshisekedi kueleza ‘majuto yake makubwa’ kwa ‘kwa ukatili wa siku za nyuma.’
Tshisekedi na mkewe walisalimiana na Mfalme Philippe na Malkia Mathilde kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji mkuu Kinshasa, jiji lenye watu wapatao milioni 15.
Siku ya Jumatatu, msemaji wa serikali ya Congo Patrick Muyaya aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ubelgiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zinaanzisha ‘ushirikiano mpya.’
“Hatusahau yaliyopita, tunatazamia yajayo,” aliongeza.
Waziri Mkuu wa Ubelgiji Alexander De Croo, ambaye anazuru taifa hilo maskini lenye watu milioni 90 pamoja na mfalme, aliunga mkono maoni hayo.
“Ni wakati wa kihistoria,” aliambia shirika la utangazaji la taifa la Ubelgiji Jumanne, akishangilia fursa ya kuunda uhusiano wa karibu zaidi katika siku zijazo.
Ukoloni wa Ubelgiji nchini Congo ulikuwa kati ya ukoloni mkali zaidi uliowekwa na mataifa ya Ulaya ambayo yalitawala sehemu kubwa ya Afrika mwishoni mwa karne ya 19 na 20.
Mfalme Leopold II, kaka wa babu mkubwa wa Philippe, alisimamia utekaji wa eneo ambalo sasa ni DRC, likitawala eneo hilo kama mali yake binafsi kati ya 1885 na 1908 kabla ya kuwa koloni la Ubelgiji.
Utawala wa kikatili –
Wanahistoria wanasema kuwa mamilioni ya watu waliuawa, kukatwa viungo vyao au kufa kutokana na magonjwa huku wakilazimishwa kukusanya mpira chini ya utawala wake.
Ardhi pia iliporwa kwa utajiri wake wa madini, mbao na pembe za ndovu.
Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Mfalme Philippe nchini DRC tangu kutwaa kiti cha ufalme mwaka 2013. Baba yake, Mfalme Albert II, alitembelea nchi hiyo mwaka 2010. Ubelgiji inajiandaa kurejesha Kinshasa jino — mabaki ya mwisho ya Patrice Lumumba — shujaa wa mapambano dhidi ya ukoloni na waziri mkuu wa kwanza wa Congo huru aliyedumu kwa muda mfupi.
Lumumba aliuawa na waasi wa Congo waliojitenga na mamluki wa Ubelgiji mwaka 1961, na mwili wake ukayeyushwa kwa tindikali, lakini jino hilo lilihifadhiwa kama nyara na mmoja wa wauaji wake, afisa wa polisi wa Ubelgiji.
Kulingana na ufalme wa Ubelgiji, mfalme pia anatazamiwa kujadili suala la kurejesha kazi za sanaa zilizoporwa wakati wa ukoloni.
Philippe anatazamiwa kujumuika katika sherehe na Tshisekedi katika bunge la Congo mjini Kinshasa siku ya Jumatano na kisha Ijumaa kutoa hotuba kwa wanafunzi wa vyuo vikuu katika mji wa kusini wa Lubumbashi.
Siku ya Jumapili, Mfalme huyo wa Ubelgiji atatembelea kliniki ya daktari wa uzazi Denis Mukwege, mshindi mwenza wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya 2018 kwa mapambano yake dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, katika jiji la mashariki la Bukavu.
Safari hiyo inakuja wakati ambapo mvutano umeongezeka kati ya Kinshasa na nchi jirani ya Rwanda kuhusu shughuli za waasi katika eneo linalokumbwa na vita mashariki mwa DRC.
Serikali ya DRC imeishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono wanamgambo walioasi wa M23, tuhuma ambayo Rwanda imekanusha.