Search
Close this search box.
Europe

Daktari wa upasuaji nchini Austria ambaye alishtakiwa kwa kukata mguu ambao haukustahili kukatwa wa mgonjwa sasa anakabiliwa na mashtaka. Mapema mwaka huu, daktari alikata mguu wa kulia wa mgonjwa mzee – ingawa mguu wa kushoto ndio uliopaswa kukatwa.

Kabla ya upasuaji huo, ambao ulifanyika mwezi Mei katika kliniki ya Freistadt, kiungo kisicho stahili kukatwa kiliwekwa alama ya kukatwa, kulingana na shirika la habari la AFP.Makosa yaligunduliwa siku mbili baadae mgonjwa alipokuwa akibadilishwa bendeji. Mgonjwa aliambiwa angehitaji kukatwa mguu wake mwingine pia.

Daktari huyo mwenye umri wa miaka 43 alishtakiwa na mahakama ya Linz na ikampata na hatia ya uzembe mkubwa. Sasa ametozwa faini ya takriban $3,053.

Mgonjwa alifariki kabla ya kesi kufika mahakamani. Mjane wake ametunukiwa $5,651, kama fidia.

Mkurugenzi wa zahanati hiyo aliomba msamaha hadharani. Daktari huyo alisema mahakamani kuwa kulikuwa na dosari katika mpangilio wa ratba na masharti katika chumba cha upasuaji.

Alisema “alifanya makosa” na kulaumu makosa ya kibinadamu, lakini akakana “uzembe kwenye kazi yake”kulingana na Kurier, gazeti la lugha ya Kijerumani lililoko Austria.Hakujua ni kwa jinsi gani aliweka alama kwenye mguu usiofaa.

Makosa kama haya ni nadra sana, lakini matukio kama haya yametokea. Mnamo mwaka wa 1995, daktari nchini Amerika aligundua akiwa katikati ya upasuaji alikuwa akikata mguu usio sahihi wa mgonjwa wa kisukari. Mgonjwa alipokea malipo ya $900,000 kutoka Hospitali ya Jumuiya ya Chuo Kikuu huko Tampa, Florida, na malipo ya $250,000 kutoka kwa Dk. Rolando Sanchez.

Comments are closed