Jumamosi ya tarehe 21 mwezi Septemba, duka la jumla la Westgate Mall lilishambuliwa na watu waliokuwa na silaha kali na kuwaua watu 72 na kuwaacha wengine wengi na majeraha.
Ni katika siku hiyo ambapo magaidi wanne waliokuwa wamevalia barakoa, walipoingia katika duka hilo lililoko katika mtaa wa kifahari wa Westlands mjini Nairobi na kuanza kushambulia watu kiholela kwa risasi.
Kabla hapo,majeshi ya Kenya (KDF) yalikuwa nchini Somalia katika zoezi la Operation Linda Nchi, zoezi hilo liliendelezwa kati ya 2011 na 2012, kumaliza shughuli za kigaidi zilizokuwa zikiendeshwa na kundi lililoharamishwa la Al- Shabab.
Baada ya mashambulzi hayo ya Westgate, kundi hilo lilidai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi baada ya Kenya kujihusisha na kampeini ya kukomesha shughuli za kundi la Al-Shabab nchini Somalia.
Uvamizi na mauaji Westage Mall uliendelea kwa zaidi ya saa 48, kamera zilizokuwa ndani ya duka zilionesha vile majambazi hao walivyotumia bunduki na grunedi katika mashambulizi hayo.
Takriban watu 71 walipoteza maisha yao, ikiwemo raia 62 na wanajeshi 5 na magaidi hao wanne. Watu wengine 200 walijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Shambulizi hilo lilitajwa kuwa baya zaidi kuwahi kufanyika nchini Kenya baada ya shambulizi la bomu katika ubalozi wa Marekani mwaka wa 1998 ambapo watu zaidi ya walipoteza maisha yao na wengine zaidi ya 400 kujeruhiwa.