Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto amewakosoa vikali wanaopinga mpango wa chanjo ya mifugo uliopangwa kuanza Januari, 2025.
Kulingana na Rais Ruto, mpango huo unatazamia kuimarisha mazao ya wakulima ili kuendana na viwango vya kimataifa wakati wa kuuza bidhaa za nyama, maziwa na ngozi katika soko za kimataifa.
Wanasiasa nchini Kenya wameonekana katika mikutano ya wakipinga mpango huo wa chanjo kwa madai haina faida kwa taifa.
Hata hivyo kauli hizo zimekejeliwa vikali na Rais Ruto ambaye amewataka wanasiasa wanaopinga mpango huo kuacha kueneza propaganda.
“Chanjo inatolewa hata kwa binadamu. Ikiwa sio hatari kuwachanja watu kwa nini iwe hatari kuwachanja wanyama?”, Rais Ruto ameuliza.
Hata hivyo, kuna baadhi ya wafugaji ambao wanapinga chanjo ya hiyo wakidai kuwa hawakupewa taarifa mapema huku wakiitaka serikali kutoa maelezo kamili kuhusu zoezi hilo.
Chanjo hiyo itakayoanza Januari tarehe 25 mwaka wa 2025, inatarajiwa kutolewa kwa ng’ombe milioni 20, kondoo na mbuzi milioni 50 kote nchini Kenya.
Sababu kuu ya kufanyika kwa chanjo yenyewe ni kutokana na serikali ya Kenya kujaribu kupiga vita ugonjwa wa Miguu na Midomo ambao kwa kiasi kikubwa umeathiri mazao ya mifugo ambazo zinaaminika ni muhimu katika kuletea wakulima faida katika soko za nje ya nchi.