Msururu wa milipuko mikali ilitikisa maeneo ya makazi ya watu wa Kyiv mapema Jumanne na kuua watu wawili, saa chache kabla ya mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi kutarajiwa kuanza tena.
Angalau milipuko mitatu mikubwa ilisikika kutoka katikati mwa mji mkuu.
Kulipopambazuka uharibifu ulidhihirika, huku mlipuko mwingine ukigonga jengo kubwa la ghorofa 16.
“Miili ya watu wawili ilipatikana, watu 27 waliokolewa,” huduma ya dharura ya Ukraine ilisema.
Mbunge wa Ukraine Lesia Vasylenko alichapisha picha ya kikosi cha zima moto wakizima moto uliokuwa ukiwaka hapo.
Vasylenko alisema mji huo ulikuwa “mahali pa kupata kahawa na kufurahia maisha. Sio tena. Mlipuko ulivuma dakika 30 zilizopita.”
Saa chache mapema, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky — alitoa hotuba mpya kupitia video akiashiria matumaini ya mazungumzo ya amani yanayoendelea.
Alidai kuwa Urusi imeanza kutambua ushindi hautakuja kwenye uwanja wa vita.
“Tayari wameanza kuelewa kwamba hawatafanikiwa chochote kwa vita,” Zelensky alisema.
Pande zote mbili bado ziko mbali katika mazungumzo hayo, huku Moscow ikiitaka Ukraine iachane na nchi za Magharibi na kutambua maeneo yaliyojitenga yanayoungwa mkono na Moscow.
Wapatanishi wa Ukraine wanasema wanataka “amani, usitishaji wa mapigano mara moja na kuondolewa kwa wanajeshi wa Urusi.”
Takriban wiki tatu baada ya msafara mkubwa wa vikosi vya Urusi kuvuka mpaka, vikosi vya Moscow vimeshambulia na kuizingira miji kadhaa ya Ukraine.
Mji mkuu wa Kyiv umezungukwa kaskazini na mashariki na karibu nusu ya wakazi wake milioni tatu wamekimbia.
Barabara za kusini pekee ndizo zimesalia wazi, mamlaka za jiji zimeweka vituo vya ukaguzi na wakaazi wanahifadhi chakula na dawa.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban watu milioni 2.8 wameikimbia Ukraine na vifo vya raia 636 vimerekodiwa, wakiwemo makumi ya watoto.
Jeshi la Urusi limekuwa likisonga polepole na kwa gharama kubwa, huku Moscow ikidharau nguvu ya upinzani wa Ukraine.
Wataalamu wengi wa masuala ya kijeshi wanaamini kuwa jeshi la Urusi sasa linahitaji muda wa kujipanga upya na kuwapelekea chakula na maji na bidhaa zingine wanajeshi wake tena, na hivyo kufungua njia ya uwezekano wa kusitishwa au kupungua kwa mapigano.
Mkuu wa jeshi wa taifa wa Urusi Viktor Zolotov ameripotiwa kukiri kuwa operesheni hiyo “haiendi haraka tunavyotaka” lakini akasema ushindi utakuja hatua kwa hatua.
Moscow imeripotiwa kugeukia Beijing kwa msaada wa kijeshi na kiuchumi — na kusababisha kile afisa mmoja wa Marekani alisema ni masaa kadhaa ya mazungumzo “ya wazi sana” kati ya maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na China.
Siku ya Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alisema taifa lake halitaki kuathiriwa na vikwazo vya Magharibi dhidi ya Urusi, huku shinikizo la Marekani likiongezeka kwa Beijing kutounga mkono kutoka Moscow.
“China haijachangia mzozo, na haingetaka kuathiriwa na vikwazo,” Wang alisema.
Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamuru vikosi vyake “kutoshambulia miji mikubwa” kulingana na msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, ambaye alitaja “kuuawa kwa raia” kuwa sababu ya kusimamisha shambulio hilo.
Aliongeza hata hivyo kuwa wizara ya ulinzi “itaendelea kudhibiti” miji mikubwa.
Wakati huo huo, washirika wa Ukraine wameweka shinikizo kwa serikali ya Putin kwa vikwazo vya kiuchumi, na Kremlin inakabiliwa na shinikizo la ndani licha ya udhibiti mkubwa wa vita.
Wakati wa matangazo ya habari ya jioni yaliyotazamwa zaidi nchini Urusi siku ya Jumatatu, mfanyakazi wa kituo hicho aliyepinga mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine, aliingia studio akiwa ameshikilia bango lililosema “Komesha vita. Usiamini propaganda.”
Mfuatiliaji wa maandamano ya upinzani alisema mwanamke huyo, mhariri katika kituo cha utangazaji cha serikali cha Channel One, alizuiliwa kufuatia ukiukaji wa mikakati ya usalama.
Makombora mjini Kyiv –
Kote Ukraine, uvamizi wa Urusi umeendelea kusababisha umwagaji damu, na kuharibu miji, maisha ya watu wengi hayatakuwa sawa tena.
“Wanasema kwamba ameungua sana, hata sitamtambua,” alilia Lidiya Tikhovska, 83, akitazama mahali ambapo mhudumu wa afya alisema mabaki ya mtoto wake Vitaliy yamelazwa kufuatia shambulizi la kombora mjini Kyiv.
“Natamani Urusi ipitie huzuni kama ile ninayohisi mimi kwa sasa, alisema, machozi yakimtiririka mashavuni.
Mwandishi wa Fox News — Benjamin Hall wa Uingereza — alijeruhiwa na kulazwa hospitalini alipokuwa akiripoti nje ya jiji, mtandao huo ulisema, siku moja baada ya mwandishi wa habari wa Marekani kuuawa kwa kupigwa risasi huko Irpin, kitongoji cha Kyiv.
Wakati huo huo wanajeshi wa Urusi wameendelea kuuzingira mji wa Mariupol, ambapo maafisa walisema karibu watu 2,200 wameuawa.
Katika hali ya matumaini kwa wakaazi wa mji huo wa bandari, zaidi ya magari 160 ya raia yaliweza kuondoka kupitia njia ya salama ya binadamu Jumatatu baada ya majaribio kadhaa kufeli.
Wakati huo huo, watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Moscow walisema vipande vya kombora la Tochka-U la Ukraine lililodunguliwa vilipenya katikati mwa jiji la mashariki la Donetsk na kuua watu 23.
Moscow ilitaja tukio hilo kama “uhalifu wa kivita” na waasi walichapisha picha za maiti zilizotapakaa mitaani.
Lakini jeshi la Ukraine lilikanusha kurusha kombora kuelekea mji huo, huku msemaji wa jeshi la Ukraine Leonid Matyukhin akisema katika taarifa yake: “Bila shaka ni roketi ya Urusi au silaha nyingine.”
Vita vya Tatu vya Dunia
Kiongozi wa Ukraine Zelensky Jumatatu alirudia wito wake kwa NATO kuweka eneo la kutoruka ndege katika nchi yake — siku moja baada ya takriban watu 35 kuuawa katika mashambulizi ya anga ya Urusi karibu na mpaka na mwanachama wa NATO Poland.
Ikiwa hautafunga anga yetu, ni suala la muda kabla ya makombora ya Kirusi kuanguka kwenye eneo letu, kwenye eneo la NATO, kwenye nyumba za raia wa NATO,” Zelensky alisema katika video.
Kuna uwezekano atarudia wito huo Jumatano atakapotoa hotuba katika mtandao kuhusu ya hali ya vita katika mabunge yote mawili ya Bunge la Marekani.
Rais Joe Biden na washirika wa Amerika wa NATO wamekataa mara kwa mara hadi sasa, wakisema kwamba jaribio lolote la kuanzisha eneo lisilo rurhusiwa kuruka kwa ndege litawaweka katika mzozo wa moja kwa moja na Urusi yenye silaha za nyuklia.
Badala yake, Washington na washirika wake wa EU wamemimina fedha na misaada ya kijeshi nchini Ukraine na kuiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi ambavyo havijawahi kushuhudiwa.
Kwa maneno ya Biden: NATO ikipigana na Urusi itakuwa “ni Vita vya Kidunia vya Tatu.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa tahadhari kwa mara nyingine tena juu ya hatari ya uwezekano wa mzozo wa vita vya nyuklia kati ya mataifa yenye nguvu za atomiki.
Alionya kwamba vita ambavyo tayari viko hatarini kuzusha “kuyumba kwa mfumo wa chakula duniani” — huku Ukraine na Urusi zikiwa ni wasambazaji muhimu wa ngano kwa mataifa kadhaa ambayo hayajaendelea.