Katika juhudi za kupunguza idadi ya mauaji, mahakama ya Misri iliomba siku ya Jumapili kwamba sheria ibadilishwe ili hukumu ya kunyongwa kwa muuaji wa mwanafunzi wa kike ipeperushwe mbashara kwenye televisheni.
Mohamed Adel alipatikana na hatia mwezi uliopita kwa ‘mauaji ya kukusudia’ ya Nayera Ashraf, mwanafunzi mwenzake wa chuo kikuu ambaye alikataa kuwa katika uhusiano nae. Adel alikiri kumuua msichana huyo katika kesi iliyosikilizwa kwa siku mbili.
Mahakama ya jinai ya Mansoura mjini Cairo, ambayo ilimhukumu Adel, iliomba bunge kubadili sheria inayoongoza adhabu ya kifo ili hukumu hiyo iweze kuonyeshwa mbashara kwenye televisheni.
Mahakama ilisema katika barua kwa bunge kwamba ‘matangazo hayo, hata ikiwa ni kwa sehemu tu yanaweza kufikia lengo la kupunguza idadi ya vifo vya wanawake nchini humo.”
Mnamo Juni, wakati video iliyodaiwa kuonyesha Ashraf akidungwa kisu mbele ya chuo kikuu chake huko Mansoura ilisambazwa mitandaoni, Wamisri walichapisha maoni yao ya kushangazwa na tukio hilo mtandaoni.
Misri, ambayo kwa mujibu wa Amnesty International ilikuwa na idadi ya tatu ya hukumu za kifo duniani kote mwaka 2021, inatoa hukumu ya kifo kama adhabu ya mwisho kwa mauaji.
Lakini utekelezaji wa hukumu ya kifo haufanywi hadharani au kuonyeshwa kwenye televisheni.
Kunyongwa kwa wanaume watatu ambao walikuwa wamemuua mwanamke na watoto wake wawili katika nyumba yao ya Cairo mnamo 1998 kulionyeshwa kwenye televisheni ya serikali, tukio la kipekee.
Katika miezi ya hivi karibuni, mauaji ya wanawake nchini Misri yamechochea hasira kubwa.
Kifo cha mtangazaji wa televisheni Shaimaa Gamal mwezi Juni kilizua taharuki katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Kijana mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela mwezi Machi kwa kumuua msichana wa shule baada ya picha zake kuwekwa mtandaoni.
Nchini Misri, sheria za mfumo dume na tafsiri kali za Uislamu zimefanya kuwa vigumu kwa wanawake kupata haki zao.
Kulingana na uchunguzi wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka wa 2015, karibu wanawake milioni nane wa Misri walikuwa waathirika wa unyanyasaji uliofanywa na wapenzi wao, familia, au watu wasiowajua katika maeneo ya umma.