Mvulana mmoja nchini Misri alijipata pabaya baada ya kumfanyia mtihani wa chuo kikuu mchezaji wa kulipwa Mostafa Mohamed, ambaye kwa sasa anachezea Mafarao katika Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON nchini Cameroon, vyombo vya habari vya serikali vilisema.
Mvulana huyo alikamatwa.
Mchezaji huyo wa kabumbu Mohamed mwenye umri wa miaka 24, yuko Cameroon na timu ya taifa ya Misri ambayo imefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya mashindano ya Afrika, huku mitihani ya kitaifa ikifanyika wiki hii nchini mwao.
Afisa wa chuo hicho aligundua kuwa sio Mohamed aliyekuwa akifanya mtihani na akawasilisha malalamiko kwa mamlaka.
Vyombo vya habari vya serikali vilimnukuu mvulana huyo aliyekuwa akimwandikia Mohamed mtihani, akisema kwamba alikuwa “akimsaidia tu Rafiki” na “tayari amefanya mitihani mitatu kwa niaba ya Mostafa Mohamed.”
Watu wengi kwenye mitandao ya kijamii nchini Misri walikejeli tukio hilo.
Mtumiaji mmoja wa Twitter aliuita “uhalifu wa kijinga zaidi katika karne ya 20 na 21” na akasema: “Wamisri milioni 100 wanaofuatilia soka katika bara zima wanajua kwamba Mostafa Mohamed yuko Cameroon.”
Haikuwa wazi kama mchezaji huyo wa kandanda alimwomba mtu mwingine kuchukua nafasi yake, na adhabu itakuwa ipi.