Misri yaichabanga Cameroon 3-1 na kutinga fainali ya AFCON

Wachezaji wa timu ya Misri wakisheherekea ushindi wao dhidi ya Cameroon (Photo by Kenzo Tribouillard / AFP)

Misri imetinga fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kuwalaza wenyeji Cameroon kwa mabao 3-1 kupitia mikwaju ya penalti uwanjani Olembe mjini Yaounde siku ya Alhamisi.

Kipa Mohamed Abou Gabal alikuwa shujaa wa Misri, akiokoa mabao kutoka kwa Harold Moukoudi na James Lea-Siliki katika mkwaju wa penalti kabla ya Clinton Njie kuwasha moto na Cameroon kupata nafasi ya mwisho na kufunga bao la kufuta machozi.

Salah, ambaye kwa kawaida ni mfungaji wa tano wa penalti, hakuhitajika kwa penalti na sasa Misri itakutana na Senegal kwenye fainali katika uwanja wa Olembe siku ya Jumapili.

Katika fainali Jumapili, Mo Salah atakuwa anakutana na mwenzake wa Liverpool, Sadio Mane, huku Mafarao hao wakiwinda taji la nane la michezo hii ya AFCON huku Senegal wakiendelea kutafuta taji lao la kwanza.

Matumaini ya Cameroon kufuzu katika fainali ya AFCON yalififia walipobanduliwa nje ya michuano hiyo mbele ya wacameroon milioni 27 waliokuwa wakitazama mchezo huo.

Cameroon watakuwa wanawania nafasi ya tatu dhidi ya Burkina Faso wikendi hii.

Siku 10 pekee zimepita tangu maafa kutokea kwenye uwanja huo, wakati watu wanane waliuawa na 38 kujeruhiwa  kwenye msongamano katika lango la kuingia uwanjani Olembe kabla ya ushindi wa 16 bora wa Cameroon dhidi ya Comoro.

Shirikisho la Soka barani Afrika lilikuwa limefunga uwanja huo kwa muda kusubiri uchunguzi wa matukio hayo, na kuuondoa mechi ya robo fainali iliyokuwa imepangiwa kuchezwa uwanjani hapo kabla ya kuruhusu michezo mingine kuendelea.

Mashabiki wachache walirejea uwanjani Olembe kwa mchezo huo wa nusu fainali ya pili, mashabiki 24,371 pekee walikuwepo katika uwanja huo wenye viti 60,000.