Wakuu wa nchi, zaidi ya mawaziri 30, maafisa wa ngazi za juu serikalini na viongozi mashuhuri kutoka Afrika wamethibitisha kuhudhuria mkutano wa awamu ya sita wa Jukwaa la Biashara la Afrika (GBF Africa) utakaofanyika Oktoba 13- 14, 2021 katika Expo 2020 Dubai.
Kauli mbiu ya mkutano huu wa biashara ni “Mabadiliko Kupitia Biashara”. Hafla hiyo inafanyika chini ya udhamini wa H.H. Sheikh Mohammed bin Rashid Al Maktoum, Makamu Rais na Waziri Mkuu wa Falme za Kiarabu na Mtawala wa Dubai.
Kati ya viongozi kutoka Afrika watakaohudhuria hafla hiyo ni Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi, Makamu wa Rais Zimbabwe Constatino Chiwenga ,Waziri Mkuu wa Jersey, Katibu Mkuu wa COMESA na zaidi ya mawaziri 30 na viongozi wa ngazi za juu Afrika, ikiwemo mawaziri kutoka Ghana, Angola, Ethiopia, Uganda Zimbabwe na Liberia, Kenya, Botswana, Ivory Coast,
Mauritius, Msumbiji ,Namibia, Niger, Senegal, Ushelisheli, Congo na Ufalme wa Lesotho pamoja na maafisa wa serikali kutoka Rwanda na Kenya.
Mheshimiwa Reem Al Hashimi, Waziri wa Falme za Kiarabu kwa masuala ya UAE na Ushirikiano wa Kimataifa na aliye pia Mkurugenzi Mkuu wa hafla ya Expo 2020 Dubai, amesema “ Mataifa mengi kutoka sehemu tofauti duniani yatakayoshiriki katika hafla ya Expo 2020 wana hamu ya kuboresha na kuimarisha uhusiano wao na Afrika,na GBF Africa itakuwa jukwaa muhimu ambapo bara Afrika linaweza kushiriki mipango na mafanikio ya biashara na kutafuta uwekezaji na upatikanaji wa suluhisho kwa changamoto wanazopitia na pia kuunda uhusiano wa biashara mpya kote duniani.