Search
Close this search box.
Africa

Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya kutumikia kifungo cha miaka 30

15
Lengai Ole Sabaya – Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha. Walipatikana na hatia kwa makosa yote matatu na kila mmoja alipewa kifungo ambacho kitatumika kwa wakati mmoja.

Akitoa hukumu hiyo leo Oktoba 15, 2021, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo, amesema ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi ya Sabaya na wenzake.

Baada ya kuwatia hatiani wakili wa Serikali alisema hakuna kumbukumbu ya makosa ya zamani ya washtakiwa wote watatu, na kuiomba Mahakama iwahukumu kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya hukumu hiyo, Wakili wa Sabaya na wenzake Mosses Mahuna, amesema hawajaridhika na hukumu hiyo iliyotolewa akidai ina upungufu mwingi. Sabaya na wenzake watatu wanatarajia kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa.

Sabaya baada ya hukumu amewataka ndugu zake wasiogope akisema kwamba Mungu yupo kazini.

“Ndugu zangu msiogope Mungu yupo kazini” amesema Sabaya.

Sabaya alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 4, mwaka huu baada ya kukamatwa Mei 27 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam. Agosti 24 mwaka huu, Sabaya na wenzake, Sylvester Nyegu, na Daniel Mbura, walikamilisha kujitetea mahakamani hapo baada ya Jamhuri kukamilisha mashahidi 11 na vielelezo vinane.

Mnamo Mei mwaka huu, Rais Samia Suluhu alimsimamisha Sabaya kama Hai DC kusubiri uchunguzi. Wakati huo Mkuu wa nchi hakutoa sababu za kusimamishwa kwa mkuu wa wilaya, ambaye wakati mmoja alikuwa mwenyekiti wa UVCCM huko Arusha.

Sabaya aliteuliwa kama DC wa Hai na Rais Marehemu John Pombe Magufuli mnamo Julai 28, 2018

Comments are closed

Related Posts