Mnyarwanda Salima Mukansanga amekuwa mwanamke wa kwanza kuwa mwamuzi wa mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika aliposimamia mechi ya Kundi B kati ya Guinea na Zimbabwe mjini Yaounde siku ya Jumanne.
Siku ya Jumatatu, taarifa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ilisema Mukansanga atasimamia mechi hiyo akiwa na maafisa wawili wa kike, Carine Atemzabong wa Cameroon na Fatiha Jermoumi wa Morocco.
Hata hivyo, wakati wasimamizi wa mechi walipoingia uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo iliyochezwa Stade Ahmadou Ahidjo katika mji mkuu wa Cameroon, waamuzi wasaidizi wote walikuwa wanaume.
CAF haikueleza mara moja kwa nini waamuzi wasaidizi walibadilishwa.
Mukansanga aliweka historia ambapo baada ya michuano 32 ya AFCON kuanzia mwaka wa 1957 ilikuwa ikisimamiwa na kuamuliwa na wanaume hadi hapo jana ambapo amekuwa mwanamke wa kwanza kusimamia mechi ya AFCON.
Hapo awali Mnyarwanda huyo alikuwa afisa wa nne wakati Guinea ilipoishinda Malawi mnamo Januari 10 mjini Bafoussam.
“Tunajivunia sana Salima kwa sababu amelazimika kufanya kazi kwa bidii ili kuwa hapa alipo leo,” alisema bosi wa waamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Eddy Maillet kutoka Ushelisheli.
“Tunafahamu kuwa kama mwanamke alilazimika kuepuka vikwazo vizito ili kufikia kiwango hiki na anastahili pongezi nyingi.
“Wakati huu si wa Salima pekee, bali kwa kila msichana mdogo barani Afrika ambaye anapenda soka na anatamanio la kuwa mwamuzi katika siku zijazo.”