Bei ya mafuta ya petroli ilipanda na kufikia kiwango cha juu zaidi nchini Morocco siku ya Alhamisi, na hivyo kuzua hasira miongoni mwa vyama vya wafanyakazi vilivyoitaka serikali ya Aziz Akhannouch kuchukua hatua ya kuwalinda watumiaji.
Madereva nchini Morocco, ambayo inategemea sana bidhaa za mafuta zinazoagizwa kutoka nje ambazo bei yake imepanda tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, lazima sasa walipe dirham 18 ($1.80) kwa lita moja ya petroli na dirhamu 16 kwa dizeli.
Katika barua ya wazi siku ya Jumatano, chama kinachoongoza Shirikisho la Wafanyakazi wa Kidemokrasia (CDT) lilitoa wito kwa Akhannouch “kuingilia kati kwa haraka ili kulinda uwezo wa ununuzi wa wafanyakazi na ya watu kwa ujumla, na kuzingatia jinsi wanavyoteseka.”
Vyama vingine vitatu vidogo viliitisha mgomo wa kitaifa wa watumishi wa ummaa, mamlaka za mitaa na sekta ya uchukuzi ili kupinga kupanda kwa gharama za maisha.
Morocco imeshuhudia kupanda kwa bei kwa miezi kadhaa na wito unaoongezeka wa kupunguzwa kwa faida ya makampuni ya nishati.
Akhannouch mwenyewe amekosolewa vikali kama mbia mkuu wa Afriquia, moja ya kampuni kuu za mafuta nchini.
Serikali hadi sasa imekataa kurejesha ruzuku ya mafuta iliyoondolewa mwaka 2015, lakini imeongeza maradufu bajeti yake ya kutoa ruzuku ya gesi ya kupikia, unga na sukari.
Pia ilisema mnamo Machi italipa dola milioni 206 kusaidia madereva wa lori ambao walifanya mgomo wa kitaifa juu ya kuongezeka kwa gharama ya mafuta.
Msemaji wa serikali Mustapha Baitas alisema Alhamisi serikali ilikuwa inachunguza kuongeza kwa malipo hayo lakini bei zinahusishwa na mazingira ya kimataifa na zinaweza kuongezeka zaidi.
Muungano wa upinzani wa Socialist Union of Popular Forces umetoa wito wa kupunguzwa kwa ushuru wa matumizi na ushuru wa juu wa mashirika.