Msimamizi wa bohari ya Bangladesh ashtumiwa kwa mlipuko ulioua takriban watu 49

Mamlaka ya Bangladesh ilishutumu msimamizi wa bohari ya makontena Jumatatu kwa kutowaambia wazima moto kuhusu hifadhi ya kemikali kabla ya kulipuka na kusababisha madhara makubwa, na kuua takriban watu 49 — tisa kati yao kutoka kwa zima moto.

Idadi ya watu waliofariki kutokana na mlipuko huo mkubwa, uliofuatia moto katika Bohari ya Kontena ya BM huko Sitakunda, inatarajiwa kuongezeka.

Baadhi ya makontena yalikuwa bado yakifuka moshi siku ya Jumatatu, zaidi ya saa 36 baada ya mlipuko huo, na kuwazuia waokoaji kuangalia eneo lililo karibu yao kwa waathiriwa.

Takriban watu 12 kati ya watu 300 waliojeruhiwa walikuwa katika hali mbaya, na walisafirishwa kwa ndege hadi mji mkuu Dhaka.

Wazima moto tisa waliokufa walikuwa wengi zaidi ambao idara imewahi kupoteza katika tukio moja katika nchi inayokumbwa na ajali za kiviwanda, ambapo viwango vya usalama ni duni na ufisadi mara nyingi hufanya viwanda hivyo kupuuzwa.

Wazima moto wawili ni miongoni mwa watu ambao bado hawajapatikana, maafisa walisema.

“Kamwe haijawahi kutokea katika historia ya idara ya zima moto, wazima moto wengi kufariki namna hii,” Purnachandra Mutsuddi, ambaye aliongoza juhudi za kuzima moto katika kituo hicho.

“Utahisi vipi unapokwenda kuwaokoa ndugu zako? Hakuna tukio chungu kama hili.”

Bohari hiyo “haikuwa na mpango wowote wa usalama wa moto” aliiambia AFP, na haikufahamisha wazima moto kuhusu kemikali, haswa peroksidi ya hidrojeni, iliyohifadhiwa kwenye ghala hiyo.

“Kama wangetujulisha, majeruhi wangekuwa wachache,” alisema.

Mutsuddi, mkurugenzi msaidizi wa kituo cha zima moto cha Chittagong, alisema kuwa mara tu wazima moto walipoingia kwenye ghala siku ya Jumamosi walimwaga peroksidi ya hidrojeni bila kujua, na kusababisha mlipuko ambao ulituma “kontena kuruka zaidi ya futi 500.”

“Kuna baadhi ya sheria za kuweka peroksidi ya hidrojeni. Tungejua hili, hatungetupa maji kamwe. Hatungewahi kupeleka gari letu ndani ya bohari,” alisema.

Huko Chittagong, mamia ya jamaa za waliopotea na waliokufa walipanga foleni hospitalini kutoa sampuli za DNA katika juhudi za kuwatambua walioaga dunia, kwani wengi wa waliofariki waliungua kiasi cha kutotambulika.

Bohari ya Kontena ya BM huko Sitakunda, mji wa viwanda ulio umbali wa kilomita 40 kutoka Bandari ya Chittagong, ni ubia kati ya wafanyabiashara wa Bangladeshi na Uholanzi na ina takriban wafanyakazi 600, na ilianza kufanya kazi mwaka wa 2012.

Mwenyekiti wake anatajwa kwenye tovuti yake kama Bert Pronk. raia wa Uholanzi, lakini AFP haikuweza kumpata ili atoe maoni yake.

Wafanyabiashara wachache wa Ulaya wanafanya kazi nchini humo.

Magazeti ya eneo hilo yalisema mmiliki wake mwingine ni afisa mkuu wa chama tawala cha Awami League kilichopo Chittagong, ambaye pia ni mhariri wa gazeti la kila siku la Kibengali.

Polisi bado hawajafungua mashtaka juu ya moto huo.

“Uchunguzi wetu unaendelea. Tutachunguza kila kitu,” alisema mkuu wa polisi wa eneo hilo Abul Kalam Azad.