Msumbiji yaondoa kitabu kinachofunza kuhusu ngono kutoka kwa mtaala wao.

Msumbiji inaondoa kutoka kwa mtaala wake wa elimu kitabu cha wanafunzi wa miaka 12 wa darasa la saba chenye masomo yenye utata kuhusu ngono.

Kitabu hicho cha sayansi ya asili kinazungumzia masuala kama vile kupiga punyeto na mwelekeo wa kijinsia.

Wizara ya elimu inasema kitabu hicho kimekuwa kikitumika tangu 2004 lakini mada hizi “zinazozua utata katika jamii” hazitafundishwa tena.

Kufundisha kuhusu masuala ya kujamiiana kwa vijana ni katika baadhi ya jamii nchini Msumbiji huchukuliwa kuwa mwiko.

Wengine pia wanaamini kuwa elimu ya ngono kwa watoto katika kundi hili inaweza kukuza ndoa za mapema na mimba za mapema.

Kitabu hicho kitaondolewa kwenye mtaala mwaka ujao lakini wizara ya elimu imezitaka shule “kutoshughulikia masuala haya.”

“Tulizungumza na mchapishaji ili kuondoa ukurasa huo,” alisema Ismael Nheze, mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Maendeleo ya Elimu.