Mwabukusi, Mashirika Ya kijamii wataka Waliombaka Msichana kukamatwa

Photo courtesy

Rais wa Tanganyika Law Society (TLS)  Boniface Mwabukusi ameanza kazi kwa kujitosa katika sakata la msichana kubakwa kwa zamu na wanaume watano.

Video hiyo iliyoanza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana Agosti 4, 2024 ikidaiwa msichana huyo amebakwa na kulawitiwa na vijana watano

Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na TLS na kusainiwa na Mwabukusi leo Jumatatu Agosti 5, 2024 imesema chama hicho kinafuatilia kwa karibu mwenendo wa sakata hilo, ili kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa

“Tukio hilo sio tu ni kinyume na sheria za nchi yetu, lakini pia ni kinyume na maadili na utamaduni wetu kama Watanzania. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kinalaani kitendo hiki kiovu na tunalitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kisheria na kuhakikisha wahalifu wote waliotenda kitendo kile na waliowezesha kutendwa kwa kitendo kile kiovu wanakamatwa na kufikishwa mahakamani mara moja, ili haki itendeke

“TLS inapinga vitendo vyote vya kikatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na iko tayari kushirikiana na vyombo vyote vya usalama na haki jinai kuhakikisha wahalifu hao wanafikishwa katika mamlaka sahihi za haki, ili kujibu mashitaka yao,”imeeleza taarifa hiyo

Taarifa ya Mwabukusi Inakujaa saa chache Tu baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelaani kitendo cha kikatili na unyanyasaji wa kijinsia kilichoripotiwa kinachomuhusu msichana (jina halijafahamika), mkazi wa Yombo Dovya, Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutoka hadharani na kuonyesha kuchukizwa na tukio hilo la udhalilishaji na ukatili.

Msichana huyo anadaiwa kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile na vijana watano wanaodai kupitia video hiyo kuwa, wametumwa na afande wakimtuhumu (msichana) kutembea na mume wa mtu.

Kipande cha video kinachosambaa mitandaoni kinaonyesha jinsi vijana hao walivyotekeleza tukio hilo ambalo tayari Polisi na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalumu, Dk Dorothy Gwajima wamelilaani.