Mwenyekiti wa Baraza la vijana wa CHADEMA (BAVICHA) jimbo la Mbeya mjini Hassan Mwamwembe, amesema anatamani Tundu Lissu aibuke kidedea kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti wa CHADEMA Taifa ili kuleta mabadiliko kwenye chama hicho.
Mwamwembe amesema hayo wakati akitoa maoni yake kufuatia uchaguzi unaoendelea katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ili kupata kiongozi mkuu wa CHADEMA kwa ajili ya kuongoza kwa miaka mingine mitano kama inavyoeleza katiba ya CHADEMA ambapo vigogo watatu wa CHADEMA wanachuana ambao ni Odero Charles Odero, Tundu Lissu na Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa BAVICHA Mbeya mjini amenukuliwa akisema kwa sasa chama kinahitaji kiongozi mwenye kuwa na maamuzi magumu kwani wapinzani na wananchi wamechoka kuwa na siasa za upinzani sizizokuwa na misimamo ya kweli hata kuwa na chaguzi zisizofuata taratibu na kuvurugwa kwa matokeo bila hatua zozote kutoka vyama vya upinzani hivyo kueleza kuwa imani yake ni Tundu Antipas Lissu anayeweza kukiongoza chama hicho kwa sasa.
Hassan Friday Mwamwembe mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA jimbo la Mbeya mjini, amesema ni imani yake Tundu Lissu atachaguliwa na mgombea mwenza wake John Heche ili kuongoza vema chama hicho kutoka kwa mtangulizi wake Freeman Aikael Mbowe.
Mpaka sasa zoezi la uchaguzi wa kitaifa ndani ya CHADEMA linaendelea mkoani Dar es Salaam ambapo macho na masikio ya wanachama, wananchi wengi, viongozi na wafuatiliaji mbalimbali wa mambo Afrika mashariki, na Duniani wanafuatilia uchaguzi huo wa chama kikuu cha upinzani (CHADEMA) Tanzania bara.