Mwanajeshi wa Burkina Faso Paul-Henri Sandaogo Damiba aliapishwa rasmi kama rais Jumatano kufuatia kupitishwa kwa ‘mkataba’ wa kurejesha serikali iliyochaguliwa mwaka wa 2025.
Damiba, Luteni Kanali mwenye umri wa miaka 41, alichukua mamlaka Januari 24, baada ya kumpindua rais mteule Roch Marc Christian Kabore.
Aliapishwa kama rais na mkuu wa vikosi vya jeshi na baraza kuu la kikatiba mnamo Februari 16.
Sherehe fupi za kurasimisha nafasi yake zilifanyika Jumatano mbele ya wawakilishi wa jeshi, vyama vya kisiasa na vyama vya wafanyikazi na mashirika ya kidiplomasia.
Damiba, akiwa amevalia sare za jeshi na bereti nyekundu, hakutoa hotuba.
Siku ya Jumanne, Damiba alitia saini kinachojulikana kama katiba ya mpito ambayo inasema uchaguzi utafanyika miezi 36 baada ya kuapishwa kwake.
Muda huu ni mrefu zaidi ya kuliko muda wa awali wa miezi 30 ambao ulikuwa umependekezwa na tume iliyoundwa na jeshi.
Mkataba huo unaeleza kuwa rais hastahili kushiriki “uchaguzi wa urais, ubunge na manispaa ambao utaandaliwa ili kukomesha kipindi cha mpito.”
Bunge la wabunge 71 na serikali ya watu 25 inayoongozwa na waziri mkuu wa kiraia itaundwa ili kuhakikisha mabadiliko hayo.
Wanachama wao pia watazuiwa kugombea nyadhfa yoyote baada ya mpito.
Moja ya nchi maskini zaidi duniani, nchi hiyo ina historia ndefu ya mizozo tangu ijinyakulie uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960.
Majirani wa kikanda wa Mali na Guinea, wamewekewa vikwazo vikali na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS). kwa kuchelewesha kurejea kwa utawala wa kiraia baada ya utekaji wa kijeshi wa hivi majuzi.
Burkina Faso, kama nchi hizo, ilisimamishwa kutoka kwa shughuli za ECOWAS baada ya mapinduzi.
Lakini iliepuka adhabu zaidi baada ya mazungumzo kati ya jeshi na wajumbe kutoka kambi hiyo.
Badala yake, iliambiwa itoe ratiba ‘inayofaa’ ‘ya kurejea kwa utaratibu wa kikatiba’.
Kabore aliondolewa madarakani kufuatia wimbi la hasira ya umma kwa jinsi alivyoshughulikia uasi wa muda mrefu wa wanajihadi.
Zaidi ya watu 2,000 wamefariki dunia tangu mashambulizi ya kwanza mwaka 2015, kwa mujibu wa shirika la AFP, huku shirika la dharura la nchi hiyo likisema zaidi ya watu milioni 1.5 wamekimbia makazi yao. Kabore amekuwa katika kizuizi cha nyumbani tangu kuondolewa kwake, licha ya wito wa kimataifa wa kuachiliwa kwake