Mwanamke kutoka Kenya anadaiwa kumuuma mwanamke mwingine vidole na kuvitafuna.

Mamlaka nchi Uhispania zinachunguza kisa ambapo mwanamke kutoka Kenya anadaiwa kumuuma mwanamke mwingine vidole na kuvitafuna.MKenya huyo alikuwa akiishi nyumba moja na mwenzake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Inadaiwa kuwa, mtuhumiwa huyo mwenye umri wa miaka 45, alimshambulia mwathiriwa kwa kumpiga na kumuuma vidole ili amtoe pepo.

Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja katika mji wa Poligono,Uhispania na mtoto mdogo wa umri wa miaka 6, aliyeshuhudia tukio hilo.

Kulingana na polisi, vurugu hiyo ilianza na ugomvi kati ya wanawake hao kabla walipoanza kupigana. Mtuhumiwa alimshtumu mwenzake ati ni mchawi na kuwa amepagawa.

Mtuhumiwa anasemekana alimpiga mwathiriwa kwa jiwe kichwani, kumsukuma chini na kumuuma vidole viwili.

Majirani waliwapigia simu polisi waliompata mtuhumiwa juu ya mwathiriwa akimpiga. Mwathiriwa mwenye umri wa miaka 48 alikuwa akivuja damu baada ya kung’atwa vidole.

Mwathiriwa alipelekwa hospitali kwa matibabu ya dharura na mtuhumiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi.