Mwanaume akamatwa kwa kumuua mwanae wa miezi 4

Maafisa wa upelelezi katika kaunti ya Murang’a wamemkamata kijana wa umri wa miaka 23 kwa madai ya kumuua mtoto wake wa miezi minne.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, mshukiwa anaonekana akimshambulia mkewe huku mtoto wao akilia sakafuni.

Kulingana na ripoti ya polisi, tukio la Jumanne alfajiri liliripotiwa na babake mshukiwa.

Mshukiwa baadaye anaonekana akimshika mtoto mchanga na kumtupa juu ya sofa. Mtoto huyo mchanga, ambaye mshukiwa anadai si mwanawe wa kumzaa, alifariki papo hapo baada ya kuanguka sakafuni.

Kufuatia tukio hilo, mshukiwa huyo anadaiwa kutishia kumuua mkewe iwapo atazungumza kuhusu kilichotokea.

Kulingana na ripoti ya polisi, mke wa mshukiwa alitoroka kutoka kwa nyumba hiyo, alikipiga kelele ndipo majirani walipokuja kumsaidia.

Mwili wa mtoto huyo umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha General Kago mjini Thika, ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.