Mwanamume mmoja nchini China amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kuchoma moto vifaa vya mtandao baada ya kukasirishwa na kasi ya polepole ya mtandao mamlaka imesema.
Mwanamume huyo, kwa jina la Lan, alikuwa kwenye mgahawa wa intaneti kusini mwa mkoa wa Guangxi Juni mwaka jana alipokasirishwa na kasi ya polepole ya mtandao katika mgahawa huo.
Lan aliamua kuharibu kisanduku cha umma kilichokuwa na nyaya za mtandao, mahakama ya eneo ilisema katika taarifa siku ya Jumatatu.
Mahakama ilisema mwanamume huyo “alitumia njiti kuwasha kitambaa moto na kukitumia kuteketeza kisanduku cha mawasiliano kwenye makutano ya barabarani.”
Moto huo ulisababisha karibu kaya na ofisi 4,000, ikiwa ni pamoja na hospitali ya umma, kukosa huduma ya mtandao kwa saa 28 hadi 50.
Lan baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa “kuharibu vifaa vya mawasiliano ya umma”
Taarifa hiyo ilizua dhihaka kubwa kwenye mtandao wa Wachina, huku mtumiaji mmoja wa mtandao wa Weibo akimwita mwanamume huyo “jitoto”