Mwanariadha mzaliwa wa Kenya anaechezea nchi ya Bahrain amepatikana amekufa nchini Kenya siku ya Jumanne, tukio ambalo limefufua kumbukumbu za mauaji ya mwaka jana ya mwanariadha aliyevunja rekodi Agnes Tirop katika mji huo huo.
Mwili wa Damaris Muthee Mutua uligunduliwa mjini Iten, eneo ambalo wanariadha maarufu duniani hufanyia mazoezi. Polisi walisema wameanzisha msako wa kumtafuta mpenzi wake mzaliwa wa Ethiopia.
Mutua, 28, alishindania Kenya kama mwanariadha mwenye umri mdogo na kushinda medali mbili za shaba katika Michezo ya Olimpiki ya Vijana ya 2010 huko Singapore na ubingwa wa riadha wa vijana wa Afrika Mashariki huko Khartoum, kabla ya kubadili uraia wake na kuwa wa Bahrain.
“Kulingana na jirani wa karibu wa Mutua, mpenzi wake alionekana nyumbani Jumapili asubuhi. Kuna uwezekano kuwa kisa hicho kilitokea Jumamosi jioni au mapema Jumapili kwasababu mwili ulikuwa umeharibika,”mkuu wa polisi wa kaunti hiyo Tom Makori alisema.
“Tumeanza msako wa kumtafuta Muethiopia huyo ambaye inaaminika alitoroka nchini.”
Mji huo wa Iten, kituo cha mafunzo kwa wanariadha mashuhuri, uligonga vichwa vya habari mwezi Oktoba Tirop alipopatikana amedungwa kisu hadi kufa nyumbani kwake.
Kuuawa kwa Tirop, nyota anayechipukia katika mbio za masafa marefu na mshindi wa medali ya shaba mara mbili ya Ubingwa wa Dunia, kulileta mshtuko kote nchini na katika ulimwengu wa riadha.
Mume wa Tirop Emmanuel Ibrahim Rotich ameshtakiwa kwa mauaji yake na bado yuko rumande lakini amekanusha mashtaka dhidi yake.
Kesi ya dhamana ya Rotich imeahirishwa mara kadhaa na sasa imepangwa kufanyika Aprili 27.