Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Mwandishi wa Uganda aliyeteswa akimbia uhamishoni - Mwanzo TV

Mwandishi wa Uganda aliyeteswa akimbia uhamishoni

Mwandishi wa riwaya Kakwenza Rukirabashaija

Mwandishi mashuhuri wa Uganda aliyeshtakiwa kwa kumtusi Rais Yoweri Museveni na mwanawe ameikimbia nchi kwa kuhofia maisha yake, wakili wake alisema Jumatano.

“Ameondoka Uganda,” Eron Kiiza, wakili wa Kakwenza Rukirabashaija, alisema.

Alisema mteja wake anayedai kuteswa gerezani, alikuwa akitafuta matibabu nje ya nchi kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Anaogopa kupewa sumu kutokana na majeraha yake na kudungwa sindano ya vitu visivyojulikana,” Kiiza alisema.

Kiiza alisema Rukirabashaija mwenye umri wa miaka 33, ambaye mwaka jana alishinda tuzo ya kimataifa ya waandishi walioteswa, alimwambia kuwa yuko nchi jirani ya Rwanda na analenga kufika Ulaya.

Rukirabashaija alizuiliwa muda mfupi baada ya Krismasi na baadaye kushtakiwa kwa “mawasiliano ya kukera” katika kesi ambayo imezua wasiwasi wa kimataifa, huku Umoja wa Ulaya ukiwa miongoni mwa wale wanaotaka uchunguzi ufanyike kuhusu ukiukaji wa haki nchini Uganda.

Alionekana kwenye runinga wikendi na kufichua makovu mgongoni mwake na sehemu nyingine za mwili wake.

“Walinipiga kwa fimbo kila mahali. nikianguka, wanapiga, nikiinuka napoteza fahamu,” alisema kwenye mahojiano na NTV Uganda.

Mashtaka dhidi yake yanahusiana na maoni yasiyofurahisha kwenye Twitter kuhusu Museveni na mwanawe Muhoozi Kainerugaba.

Alimtaja Kainerugaba, jenerali ambaye Waganda wengi wanaamini kuwa anajiweka katika nafasi ya kuchukua uongozi kutoka kwa babake mwenye umri wa miaka 77, kuwa ‘mnene’ na ‘mwenye mbwembwe’.

Aliachiliwa kwa dhamana mnamo Januari baada ya kukaa rumande kwa karibu mwezi mmoja, kesi yake itaanza Machi 23.

Hakimu mkuu Douglas Singiza alikataa kulegeza masharti ya dhamana ya Rukirabashaija, ambayo ni pamoja na kuzuiliwa kwa paspoti yake na amri ya kutozungumza na wanahabari.

Katika mahojiano ya televisheni Jumamosi — yaliyofanywa licha ya masharti ya dhamana — mwandishi alisema alilazimishwa kucheza bila kupumzika kwa siku kadhaa na alidungwa mara kadhaa na kitu kisichojulikana.

Rukirabashaija alisema kwenye Twitter Jumatano kwamba mtoto wa Museveni, Kainerugaba “aliamrisha mateso yangu”

Kiiza alisema mteja wake alikuwa na lengo la kwenda Ujerumani kwa matibabu.

“Aliniambia yuko Rwanda na anaenda nchi nyingine na kuelekea Ulaya,” Kiiza aliongeza.

Uganda na Rwanda hivi karibuni zimerekebisha uhusiano wao baada ya miaka mingi ya uhasama, na mpaka wa ardhi ulifunguliwa tena mwezi uliopita.

Kainerugaba alitweet kuwa amezungumza na Rais wa Rwanda Paul Kagame ambaye alimwambia kuwa mwandishi huyo hayupo nchinihumo.

Siku ya Jumatatu, EU ilitoa taarifa ikielezea wasiwasi wake kuhusu “ongezeko kubwa la ripoti za mateso, kukamatwa kiholela, kutoweka kwa nguvu, unyanyasaji pamoja na mashambulizi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu, wanachama wa upinzani na wanaharakati wa haki za mazingira.”

Museveni, ambaye alichukua madaraka mwaka 1986 na aliwahi kusifiwa kuwa mpenda mageuzi, amekabiliana na wapinzani na kubadilisha katiba ili kujiruhusu kugombea tena na tena.

Waandishi wa habari wameshambuliwa, mawakili kufungwa, waangalizi wa uchaguzi kufunguliwa mashtaka na viongozi wa upinzani kunyamazishwa.

Mwanaharakati na mwandishi wa Uganda Stella Nyanzi, ambaye alifungwa 2019 baada ya kuchapisha shairi  kuhusu Museveni, pia alikimbilia Ujerumani mapema mwaka huu.

Rukirabashaija alijishindia sifa kwa riwaya yake ya kejeli ya 2020 ‘The Greedy Barbarian”, ambayo inaelezea ufisadi wa hali ya juu katika nchi ya kubuni.

Alitunukiwa Tuzo ya PEN Pinter mwaka wa 2021 kwa Mwandishi wa Kimataifa wa Ujasiri, ambayo hutolewa kila mwaka kwa mwandishi ambaye ameteswa kwa kusema juu ya imani zao.

Rukirabashaija amekuwa akikamatwa mara kwa mara tangu riwaya yake “The Greedy Barbarian” kuchapishwa na kusema aliteswa hapo awali alipokuwa akihojiwa na ujasusi wa kijeshi.