Mwenyekiti wa zamani wa IEBC Wafula Chebukati afariki

Chebukati alifariki jana Alhamisi jioni wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda. Alihudumu kama Mwenyekiti wa IEBC kati ya mwaka 2017 na 2023.

Wafula Chebukati, the Chairman of Independent Electoral and Boundaries Commission (IEBC), attends a media briefing on the voter register at Bomas of Kenya in Nairobi, Kenya, on June 20, 2022. (Photo by Yasuyoshi CHIBA / AFP)

Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ameaga dunia.

Chebukati alifariki jana Alhamisi jioni wakati akipokea matibabu katika hospitali moja jijini Nairobi.

Alikuwa na umri wa miaka 63.

Chebukati alisimamia IEBC kwa kipindi cha miaka 6 baada ya kuteuliwa kwenye wadhifa huo mwezi Januari mwaka 2017.

Aliondoka kwenye wadhifa huo mwezi Januari mwaka 2023 baada ya kusimamia chaguzi tata za mwaka 2017 na 2022.

Chebukati na makamishna Prof. Abdi Guliye na Boya Molu ndio pekee waliohudumu kwa kipindi cha miaka sita.

Chebukati alikuwa mwanasheria aliyejizolea tajiriba ya miaka 37 katika masuala ya sheria nchini.

Rais William Ruto na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula ni miongoni mwa walioomboleza kifo chake.