Mwili Wa Mchezaji Christian Atsu Watua Nchini Ghana,Wapokelewa Na Majeshi.

Mwili wa mchezaji wa timu ya taifa ya Ghana na kilabu ya Hatayspor nchini Uturuki Christian Atsu uliwasili nchini Ghana Jumapili jioni.


Baada ya ndege iliyokuwa imebeba Jeneza lake Christian Atsu kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kotoko,makamu wa rais Mahamudu Bawumia alikuwa katika uwanja huo kuupokea mwili huo huku wanajeshi wakiubeba.


Makamu wa rais Mahamudu Bawumia alielezea jinsi kufariki kwake Atsu ni pigo kwa taifa la Ghana ikizingatiwa kuwa walikuwa na matumaini tele kwake kuliwakilisha Taifa katika soka la ughaibuni.


“Kila wakati tulikuwa tunaomba kwamba Atsu apatikane,ni msiba mkubwa zaidi kwa Ghana.Alikuwa kielelezo kikuu kwa vipaji chipukizi vya soka na jamii kwa ujumla”alisema Bawumia.


Atsu mwenye umri wa miaka 31,alipatikana ameaga dunia katika vifusi vya nyumba yake mjini Hatay Uturuki kufuatia tetemeko la ardhi lilotokea Februari 6 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 4,000 huku maelfu ya wengine wakipata majeraha.


Kulikuwa na ripoti awali ambazo zilidokeza kuwa Atsu alikuwa ameokolewa ila ikabainika kuwa zilikuwa za uwongo baada ya mwili wake kupatikana katika vifusi vya nyumba yake.


Atsu aliichezea timu ya taifa ya Ghana katika mechi 65 na kuisaidia kufika katika fainali ya kombe la bara afrika 2015.


Baadhi ya vilabu ambavyo amesakatia barani ulaya ni Chelsea,Everton,Bournemouth na Newcastle.


Mkewe Atsu Marie-Claire Rupio ambaye kwa pamoja wamejaliwa kupata watoto watatu walijiunga na mashabiki wa ligi kuu uingereza katika mechi kati ya Newcastle na Liverpool kumpa heshima gwiji huyo wa soka.