Mwimbaji wa RnB kutoka Marekani R. Kelly amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kutumia hadhi yake kuendesha mpango wa kuwadhalilisha kingono watoto na wanawake.
Adhabu hiyo, kali zaidi ya miaka 25 jela ambayo waendesha mashitaka walikuwa wameagiza, imezima ustaa wa muda mrefu kwa nyota huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 55.
“Ninashukuru kwamba Robert Sylvester Kelly hayupo na atasalia mbali na hataweza kumdhuru mtu mwingine yeyote,” mwathiriwa Lizzette Martinez aliwaambia waandishi wa habari nje ya mahakama ya shirikisho ya Brooklyn.
Mnamo Septemba, msanii huyo wa “I Believe I Can Fly’ alipatikana na hatia katika mashtaka yote tisa aliyokabiliwa nayo, yakiwemo makubwa zaidi ya ulaghai.
“Umma lazima ulindwe dhidi ya tabia kama hizi,” jaji Ann Donnelly alisema, akitoa hukumu hiyo.
Breon Peace, wakili wa Marekani wa Wilaya ya Mashariki ya New York alisifu hukumu hiyo kama ‘matokeo muhimu” kwa waathiriwa 11 ambao walitoa ushahidi kuhusu “unyanyasaji wa kutisha na wa kusikitisha waliovumilia.”
Mawakili wa Kelly walitaka hukumu iwe nyepesi na isiyozidi miaka 17.
Wakili Jennifer Bonjean alimweleza hakimu kuwa mteja wake alitokana na malezi mabaya ambayo yalijumuisha kudhulumiwa kingono alipokuwa mtoto.
“Bw Kelly anakataa kuwa yeye ni mtu mbaya kama alivyoelezwa” Bonjean alisema, baadaye akiwaambia wanahabari nje ya mahakama kwamba angekata rufaa.
Kelly, mshindi wa Tuzo ya Grammy mara tatu, alichagua kutozungumza katika kesi hiyo kutokana na kesi na kuwa kuna kesi nyingine inayosubiri.
Hukumu hiyo inakuja mwezi mmoja tu kabla ya uteuzi wa mahakama kuanza katika kesi tofauti ya Kelly, iliyocheleweshwa kwa muda mrefu ya shirikisho huko Chicago mnamo Agosti 15. Katika kesi hiyo, Kelly na washirika wake wawili wa zamani wanadaiwa kuficha ukweli kuhusu kesi ya ponografia ya 2008 na kuficha miaka mingi ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto.
Mwanamuziki huyo ambaye aliwahi kutawala RnB pia anakabiliwa na mashtaka katika maeneo mengine mawili ya serikali.
Hukumu ya Kelly mjini New York ilionekana sana kama hatua muhimu kwa vuguvugu la #MeToo: Ilikuwa ni kesi ya kwanza kuu ya unyanyasaji wa kingono ambapo washtaki wengi walikuwa wanawake Weusi.
Ilikuwa pia mara ya kwanza kwa Kelly kukabiliwa na matokeo ya uhalifu kwa unyanyasaji ambao kwa miongo kadhaa alisemekana kuwafanyia wanawake na watoto.
Waendesha mashtaka walipewa jukumu la kuthibitisha kuwa Kelly ana hatia ya ulaghai, shtaka la shirikisho ambalo kwa kawaida linahusishwa na makundi ya uhalifu yakujipanga ambayo yalimwonyesha Kelly kama bosi wa biashara ya washirika waliofanikisha unyanyasaji wake dhidi ya watoto.
Wakiwaita mashahidi 45 wakiwemo waathiriwa 11 kwenye mahakama hiyo,waliwasilisha kwa uchungu muundo wa uhalifu ambao wanasema msanii, jina kamili Robert Sylvester Kelly alitekeleza kwa miaka mingi bila kuadhibiwa, akitumia umaarufu wake kuwawinda watu wasio na uwezo.
Ili kumtia hatiani Kelly kwa ulaghai, majaji ilibidi wampate na hatia ya angalau vitendo viwili kati ya 14 vya kudhamiria uhalifu wa msingi kwa muundo mpana wa makosa haramu.
Ushahidi mkali uliokusudiwa kuthibitisha vitendo hivyo ni pamoja na ubakaji, dawa za kulevya, kifungo na ponografia ya watoto.
Wengi waliomshtaki Kelly walielezea matukio ambayo mara nyingi yalikuwa sawa kati yao wote: Wengi wa waathiriwa walisema walikutana na mwimbaji kwenye matamasha au maonyesho na walikabidhiwa karatasi zenye nambari za simu za Kelly kutoka kwa wasaidizi wake.
Wengi walisema waliambiwa angeweza kuwasaidia kutimiza matamanio yao ya tasnia ya muziki.
Lakini waendesha mashitaka walidai kwamba wote badala yake waliingizwa katika ulimwengu wa Kelly — waliandaliwa kufanya ngono kwa matakwa yake Kelly.
Video vya kikatili vya ngono vilivyofanyiwa wanawake hao na watoto zilichezwa mahakamani.
Msingi wa kesi ya serikali ilikuwa uhusiano wa Kelly na mwimbaji marehemu Aaliyah.
Kelly aliandika na kutoa albamu yake ya kwanza – Age Ain’t Nothin’ But A Number — kabla ya kumuoa kinyume cha sheria akiwa na umri wa miaka 15 tu kwa sababu alihofia kuwa amempa ujauzito.
Meneja wake wa zamani alikiri mahakamani kumhonga mfanyakazi ili kupata kitambulisho ghushi kilichoruhusu ndoa kati yao wawili, ambacho kilibatilishwa baadaye.