Naibu rais wa Kenya ashinikiza kuwa na eneo moja la starehe katika kila mji kupambana na ulevi

Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua

Naibu Rais Rigathi Gachagua amewataka magavana kutoa leseni kwa baa moja tu katika kila mji haswa kwa eneo la kati karibu na Mlima Kenya.

Gachagua alisema unywaji wa pombe haramu umefikia viwango vya wasiwasi na unatishia kuondoa kizazi cha vijana.

Aidha aliwaamuru maafisa wa utawala kupambana na uuzaji na ubugiaji wa pombe haramu ambao umekithiri katika eneo la Mlima Kenya.

“Hatutakubali hali ambapo vijana wanauawa au kukosa tija kwa sababu ya unywaji wa pombe haramu. Ni lazima wasimamizi wakomeshe ulevi na utumizi wa mihadarati. Utawala wa Ruto hautajadiliana kuhusu jambo hili la kusikitisha,” akasema.

“Lazima wasimamizi wote warejee kazini sasa kwani ulevi unazidi kuwa tishio sasa na hali hii lazima ishughulikiwe madhubuti,” aliongeza.

Naibu Rais alizungumza mjini Murang’a siku ya Alhamisi wakati wa uzinduzi wa mpango wa kaunti ya utoaji wa fedha. Alipokuwa akichangia buraza na masomo, alimshukuru Gavana Irungu Kang’ata kwa mpango huo.

Gachagua aliandamana na viongozi mbalimbali wa kisiasa akiwemo Gavana Kang’ata, Seneta Joe Nyutu, Mwakilishi wa Wanawake Betty Maina na Mbunge wa Maragua Mary Wamaua. Wengine ni pamoja na wabunge Joseph Munyoro (Kigumo), Erick Wa Mumbi Mwangi wa Mathira.

Viongozi hao waliahidi kuunga mkono azma ya Naibu Rais ya kutokomeza dawa za kulevya katika eneo hilo.
Wakati uo huo, Gachagua amewataka polisi na maafisa wa utawala kutoshiriki siasa, bali wazidishe juhudi za kudhibiti hali ya unywaji pombe haramu na mihadarati.

Alisema kazi yao kwa sasa ni pamoja na kuendesha programu za upandaji miti.
Aliongeza kuwa mipango ya kurahisisha na kurekebisha sekta ndogo za chai, kahawa na maziwa inaendelea.
Aidha, DP alisema miradi ya maendeleo iliyokwama itaanza tena hivi karibuni kwa kuwa serikali inakusanya fedha za kulipa madeni inayodaiwa na wakandarasi.