Nairobi yatajwa miongoni mwa maeneo 50 bora zaidi Duniani kwa mwaka 2022 na Jarida la Time

Mji mkuu wa Kenya Nairobi umetajwa katika orodha ya World’s Greatest Places 2022 iliyotolewa na Jarida la Time.

Orodha hiyo ilitayarishwa na mtandao wa kimataifa wa waandishi na wachangiaji wa jarida hilo la Marekani, kwa kuangalia nchi ambazo hutoa uzoefu mpya na wa kusisimua.

Nairobi ni mojawapo ya maeneo 50 kwenye orodha ya “mji mkuu wa kitamaduni,” Time ikielezea mji mkuu wa Kenya kama “mji mkuu wa utalii duniani.”

Jarida hili linataja matukio mengi ya kusisimua ya Nairobi, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Sanaa ya Kisasa ya Nairobi (NCAI), Eden Nairobi, Kwetu Nairobi, na Curio Collection by Hilton kama baadhi ya sababu za kuchaguliwa kwake.

Time imetaja Barabara ya Nairobi Expressway iliyojengwa hivi karibuni: mradi wa $650 milioni ambao hutoa ahueni ya muda mrefu kutokana na msongamano katikati ya jiji, ili wakazi na wageni waweze kuufikia kwa urahisi na haraka zaidi kuliko hapo awali.

Maeneo mengine 50 katika orodho hiyo yanajumuisha  maeneo ambayo hayajatembelewa na watalii sana lakini Times inasema kinachounganisha maeneo yote ni kwamba “yana ustawi, yanakua na kubadilika, yanapanga njia ya kufufua uchumi na kuwekeza katika miradi endelevu.”

Baadhi ya maeneo mashuhuri kwenye orodha ya Time ni pamoja na Ras Al Khaimah (UAE), Park City (Utah), Visiwa vya Galåpagos, Dolni Morava (Jamhuri ya Czech), Seoul, Great Barrier Reef (Australia), Doha (Qatar), Detroit (USA), Kerala (India), The Arctic, Ahmedabad (India), Toronto (Canada), València (Hispania),

Maeneo mengine ni Devon (England) Bali (Indonesia), International Space Station, Kyushu Island (Japan), Miami (USA), Calabria (Italia), Marseilles (Ufaransa), na Jamaica.