Shirika la Kenya Railways, limetangaza nyongeza ya nauli za treni.
Kwenye taarifa kwa umma shirika hilo lilifafanua kwamba nauli zilizoongezwa ni za safari ndefu za treni ya Madaraka Express, safari fupi za Madaraka express, safari za treni katika eneo la Nairobi, safari za treni hadi Kisumu na zile za kuelekea Nanyuki.
Usimamizi wa shirika hilo ulielezea kwamba nyongeza hiyo imechochewa na ongezeko la bei ya mafuta na bidaa za petroli ambalo limeongeza pakubwa gharama yao ya kuhudumu.
Nauli mpya zitaanza kutozwa Januari Mosi mwakani na tayari wateja ambao hununua tiketi za usafiri mapema kwa siku 60 wanaweza kuona mabadiliko hayo ya nauli.
Wasafiri wa “first class” kutoka Nairobi kuelekea Mombasa kwenye Madaraka Express watakuwa wanalipa shilingi, 4500.
Kutoka Nairobi hadi Mariakani nauli ni 4310, kutoka Nairobi hadi Miasenyi 3680 na hadi Mtito Andei nauli itakua 2240.
Kutoka Nairobi hadi Mombasa kwenye “Economy Class” nauli ni shilingi 1500, kutoka Nairobi hadi Mtito Andei ni shilingi 740 na hadi Voi ni shilingi 1050.
Watoto wa chini ya miaka mitatu hawatatozwa nauli yoyote, watoto wa kati ya miaka mitatu hadi 11 ambao watakuwa wanasafiri na wazazi au walezi watalipa nusu ya nauli huku wale wa umri wa zaidi ya miaka 11 wakilipa nauli yote kama kawaida.