Je, una uzito gani wa mwili, ushawahi kuwa na uzani wa zaidi ya kilo 100?
Katika nchi ndogo ya kisiwa ya Nauru, takriban 94.5% ya idadi ya watu nchini humo wana uzito wa kupita kiasi.
Nauru inajulikana kuwa na viwango vya juu zaidi vya wakaazi wanene ulimwenguni kote, ikiwa wengi wa waNauru wana uzito wa takrriban kilo100.
Jamhuri ya Nauru ni kisiwa kidogo kilichoko katika bahari ya Pacific, ni nchi ya tatu kwa udogo baada ya Vatican City na Monaco, ikiwa na wakazi wapatao 10,000.
Nauru ni mwanachama wa miungano ya Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Madola.
Unene wa kupita kiasi nchini Nauru umekuwa tatizo kubwa katika taifa hilo, huku Shirika la Afya Duniani WHO likikadiri kuwa 94.5% ya wanauru ni wanene kupita kiasi.
Kuna mambo mengi ambayo yamechangia tatizo hilo la uzito wa kupitiliza. Katika miaka ya nyuma wanauru walikula vyakula asili na vilivyopatikana kwa urahisi nchini mwao, ikiwa ni samaki kwa wingi, mihogo na nduma pamoja na mboga, nazi na matunda.
Ila baada ya Nauru kupata uhuru mwaka wa 1968 na uchumi wa nchi kufanya vyema kutokana na uchimbaji wa madini ya fosfati ambayo hupatikana kwa wingi, utajiri mkubwa uliokuja baada ya uchimbaji huo uliwafanya vijana wengi ambao wangefanya kazi katika viwanda na kuendeleza kilimo na uvuvi kuhamia mataifa mengine.
Kukosekana kwa nguvu kazi baada ya kuondoka kwa vijana wengi na kuharibika kwa ardhi baada ya uchimbaji wa fosfati, Nauru ililazimika kuagiza chakula kilichosindikwa, chenye sukari na mafuta mengi kutoka nchi jirani za New Zealand na Australia.
Hata baada ya utafiti kufanywa na kuonesha kuwa uzito wa kupita kiasi unasababisha magonjwa ya sukari, si rahisi kwa waNauru kubadili mtindo wao wa maisha kwasababu unene unaonekana kama ishara ya utajiri.
Nauru ina kiwango cha juu zaidi cha kisukari kati ya watu wazima wa umri wa miaka 55 hadi 64 kote duniani. 31% ya waNauru wanaugua kisukari. 71% ya watu ni wanene na 97% ya wanaume wanauzito wa kupita kiasi.